Majaliwa awapa 5 Tume ya Madini
DAR ES SALAAM: WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Tume ya Madini ipo thabiti katika kuhakikisha taifa linafaidika na rasilimali ya madini.
Amesema hayo leo, alipotembelea banda la Tume ya Madini kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini unaotamatishwa leo Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
“Tuna imani kubwa na hatuna mashaka na utendaji wenu kama taasisi kwenye usimamizi wa sekta ya madini hasa katika kuhakikisha Watanzania wananufaika,’”amesema Waziri Mkuu .
Awali akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, Ofisa Biashara wa Tume ya Madini Issa Lunda ameelezea mikakati ya serikali katika kuhakikisha Watanzania wananufaika katika sekta ya madini kupitia ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta hiyo na huduma zinazotolewa na maabara ya Tume ya Madini .
Pia mesema kumekuwepo na mwitikio mkubwa wa Watanzania kwenye utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini kutokana na elimu ambayo imekuwa ikitolewa mara kwa mara na tume.