Majaliwa: Hakuna uwekezaji utakaokwama

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha wawekezaji wanapata faida na hakuna mwekezaji atakayekwama kwa namna yoyote.

Majaliwa alisema hayo Kisemvule wilayani Mkuranga mkoani Pwani wakati alipotembelea na kuweka jiwe la msingi la Kiwanda cha Kutengeneza Mabati cha Lodhia.

Alisema serikali imeweka mazingira mazuri ya kuwekeza kwa wawekaji wa ndani na wa kutoka nje na kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza wenye nia ya kuwekeza hawapati shida wala vikwazo vyovyote.

“Tunatambua uwekezaji huu, tunaheshimu uwekezaji huu, tutakuunga mkono kwenye uwekezaji huu, pale unapopata tatizo usisite kutuambia,” alisema Majaliwa.

Alipongeza Kundi la Kampuni za Lodhia kwa kuunga mkono juhudi za serikali la kupunguza ukubwa wa tatizo la ajira na akasema Watanzania wana uwezo wa kufanya kazi hivyo hakuna sababu ya kuajiri watu kutoka nje ya Tanzania.

Alisema vijana wa Kitanzania wanaajirika na wanafanya kazi kwa bidii hivyo viwanda vya Lodhia viendelee kuajiri ili kupunguza watu waliopo mitaani wakitafuta ajira.

Alisema kampuni hiyo ni miongoni mwa zinazolipa kodi kubwa ikilipa zaidi ya Sh bilioni 40 kwa mwezi hivyo kuchangia katika pato la serikali.

Waziri Mkuu alisema kiwanda hicho kinachozalisha chuma zikiwamo nondo, ni kikubwa kuliko viwanda vyote alivyotembelea kuweka mawe ya msingi.

“Uwepo wa viwanda vya nondo, plastiki, mabomba ya maji na bati itasaidia bidhaa kwani zitapatikana hapa nchini badala ya kuagiza nje na pia zina ubora bado eneo dogo kufikia kiwanda cha Afrika Mashariki itafikia hatua hiyo na kuwa kiwanda kikubwa hapa Afrika Mashariki,” alisema Waziri Mkuu.

Mwenyekiti na mwanzilishi wa kampuni hiyo, Haroun Lodhia alisema kiwanda hicho kinalipa zaidi ya Sh bilioni 22 kwa ajili ya umeme na gesi na baadaye watakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 40,000 za chuma kwa mwezi.

Lodhia alisema kwa siku za baadaye watazalisha umeme wao wenyewe na wataanza kuzalisha megawati tano na wanaishukuru serikali kwa kuwawekea mazingira mazuri kuendesha shughuli zao.

Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega alisema kutokana na uwekezaji uliopo kwenye Wilaya ya Mkuranga na wingi wa magari yanayokwenda mikoa ya Kusini, wanaomba barabara ya Kusini iwe na njia nne.

Ulega alisema ni muhimu barabara kuanzia Mbagala Rangi Tatu kwenda Mwandege Vikindu na kuendelea ipanuliwe ili bidhaa zisafirishwe kwa urahisi.

Habari Zifananazo

Back to top button