WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mbio za Maendeleo Bank Marathon zitakazofanyika Septemba 2, 2023.
Meneja Miradi wa benki hiyo, Norah Kimambo amesema Dar es Salaam leo kuwa mbio hizo zina lengo la kukusanya Sh milioni 200 kwa ajili ya kununua vitanda vya watoto njiti katika Hospitali ya KMC pamoja na ukarabati wa Kituo cha Diakonia cha Kilutheri cha Mtoni kinacholea watoto wenye ulemavu wa akili.
Amesema wametoa mwaliko kwa Waziri Mkuu kwa kuwa mara nyingi huwa anazungumzia kwa uzito suala la afya ya watoto, ndio maana wameamua kuunga mkono juhudi zake kwa vitendo.
“Ni mkakati wa kuweka uzito wa tukio hili kumualika Waziri Mkuu kwa kuwa ni mtu muhimu katika sekta hii, huwa anaizungumzia kwa uzito kwa hiyo na sisi tukaona itakuwa vizuri kuiunga mkono serikali katika harakati zake hizi,” amesema Norah.
Amesema kuwa tofauti na Waziri Mkuu pia wametoa mwaliko kwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pindi Chana pamoja na wadau mbalimbali wanaofanya biashara na benki hiyo.