WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kampeni ya huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samia itasaidia kuboresha upatikanaji wa haki kwa wasiojiweza hasa wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu.
Majaliwa amesema hayo Dodoma jana wakati anazindua kampeni hiyo itakayotekelezwa kwa miaka mitatu kuanzia Machi mwaka huu hadi Desemba 2025.
Alisema kampeni hiyo itasaidia kuongeza uelewa wa sheria na upatikanaji haki, mifumo ya utoaji haki, masuala ya kisheria na haki za binadamu kwa kushirikiana na taasisi za serikali, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo katika utoaji huduma kwa wananchi.
“Vilevile, itachangia kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato cha mmoja mmoja na kuleta utengamano wa kitaifa,” alisema Majaliwa.
Alitaja faida nyingine ya kampeni hiyo ni kusaidia kuimarisha mfumo wa utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria katika ngazi zote yaani kuanzia serikali kuu hadi serikali za mitaa.
“Ushiriki wa wadau wanaojihusisha na huduma ya msaada wa kisheria utaongezeka kwa asilimia 80 katika ngazi za Serikali Kuu hadi Serikali za Mitaa,” alisema Majaliwa.
Aliagiza Wizara ya Katiba na Sheria iweke mfumo mzuri wa kushughulikia changamoto za kisheria zitakazoibuliwa wakati wa kampeni hiyo.
Alihimiza Watanzania waitumie kampeni hiyo kutoa taarifa kuhusu uwepo wa watu au vikundi vya watu ambao ama wanajihusisha na ukatili wa kijinsia hususani kwa watoto.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro alisema kampeni itakayotekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar itatoa elimu katika maeneo ya migogoro ya ardhi, mirathi, ndoa, sheria ya mtoto katika maeneo ya ukatili wa kijinsia na maadili.
Dk Ndumbaro alisema watatumia mawakili 5,000, askari polisi 165, askari magereza 112 ambao wamepewa mafunzo maalumu ya huduma ya msaada wa kisheria katika kampeni ya miaka mitatu kuanzia 2023 hadi 2025 inayojulikana kwa jina la ‘Mama Samia’.
Alisema kampeni ilianza Dodoma jana hadi Mei 9, 2023 na mkoa huo utafuatiwa na mikoa ya Shinyanga, Manyara, Ruvuma na mikoa mingine.