RUVUMA: WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa jamii kuwa iendelee kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita na Rais Samia Suluhu Hassan katika kupinga vitendo vya ukatili kwa watoto kwani vinasababisha watoto wengi kukimbia familia zao na kukosa makao maalumu.
Alisema hayo jana wakati wa hafla ya chakula cha mchana na watoto wanaolelewa katika makao ya kulelea watoto ya Swacco yaliyoko Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma na kuwataka maofisa ustawi wa jamii watekeleze kikamilifu wajibu wao ikiwemo kutambua vituo au makao na kutatua changamoto za ustawi zinazoikabili jamii na kutoa msaada wa kisaikolojia na afya ya akili kwa walengwa.
“Jamii na Watanzania kwa ujumla kila mmoja ashiriki katika kulinda haki na ustawi wa watoto wetu. Hii ni nguvukazi ya taifa letu hivyo basi, ulinzi na usalama wa watoto ni jukumu letu sote.
“Mamlaka zinazohusika ziendelee kusimamia, kufuatilia na kuratibu vyema huduma za makao ya watoto zinazotolewa na serikali na wadau mbalimbali,” alisema.
Majaliwa aliutaja pia uongozi wa mkoa na mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha wanaweka utaratibu wa kuwatembelea wadau wanaoshirikiana na serikali kutoa huduma kwa wenye uhitaji ili kutambua changamoto walizonazo na kuzitafutia ufumbuzi, pamoja na kuwapa uelewa wa mipango na mikakati ya serikali kuhusu huduma za ustawi wa jamii.
Aliitaka wizara inayohusika na masuala ya ustawi wa jamii iendelee kushirikiana na wadau kuongeza kasi ya utoaji elimu ya malezi chanya kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla ili kuwa na nguvu kazi yenye tija kwa taifa.
Wakati huo huo, Majaliwa alitoa wito kwa Watanzania wote wahakikishe kuwa watoto wote wenye ulemavu wanapewa fursa ya kupata huduma za jamii ikiwemo elimu na waache tabia za kuwaficha ndani badala yake washirikishe mamlaka ikiwemo viongozi wa mitaa, vijiji, kata na wilaya ili kupata msaada.
Kwa upande wake, Meneja wa Kituo hicho, John Chinguku alisema kituo hicho kilianzishwa Septemba 29, 2000 na Regina Chinguku akiwa na lengo la kusaidia na kuunga mkono jitihada za serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kupunguza changamoto za watoto yatima na wale wanaoishi kwenye mazingira hatarishi kwa kuwapatia huduma za afya, elimu, chakula, mavazi na makazi. Kwa sasa kituo kina watoto 50.