Majaliwa: ‘Nilikuwa nakusanya pesa nikasome udereva’
MAJALIWA ni jina linalovuma ndani na hata nje ya nchi baada ya kuwa ‘raia wa kwanza’ aliyeshuhudia na kushiriki kikamilifu uokoaji wa watu katika ndege ya Precision iliyopata ajali mjini Bukoba na kusababisha vifo vya watu 19.
Ajali ya ndege hiyo aina ya ATR 42-500 yenye namba za usajili 5H-PWF, ilitokea Novemba 6 asubuhi wakati ikitua katika Kiwanja cha Ndege cha Bukoba. Ilikuwa na watu 43, abiria wakiwa 39, marubani wawili na wahudumu wawili.
Idadi ya waliookolewa ni 24 wakiwamo abiria 22 na wahudumu wa ndege wawili ambao kijana Majaliwa ana mchango mkubwa katika kuwaokoa.
Waliopoteza maisha ni abiria 17 na marubani wawili, ambao pia kijana huyu alifanya juhudi kuwaokoa, lakini haikuwezekana kutokana na sababu anazoeleza kupitia mahojiano na HabariLEO. Kijana huyu mwenye umri wa miaka 20, unapozungumza naye, taswira yake ya nje inamwonesha alivyo mtulivu.
Katika mahojiano na HabariLEO, anadhihirisha kuwa kijana anayesikiliza, kujibu maswali kwa umakini, unyenyekevu na nidhamu. Hata alipokuwa akitoka kwenye Uwanja wa Kaitaba juzi akiongozana na maofisa wa jeshi baada ya shughuli ya mazishi ambayo alitangazwa kuwa shujaa, alidhihirisha nidhamu yake kuitikia kwa heshima sauti za umati wa watu uliokuwa ukimshangilia kwa kutaja jina lake ‘Majaliwa…Majaliwa asante.”
Kabla ya hapo, alitambulishwa kwa wananchi uwanjani hapo na kisha kusalimiana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati wote akibubujikwa na machozi. Mapito ya Majaliwa Huyu ndiye Majaliwa Jackson, kijana aliyetenda makuu katika historia ya mashujaa wa nchi. Kijana aliyeishia kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Rumuli iliyopo mjini Bukoba, mkoani Kagera.
Darasa la kwanza hadi la saba alisoma Shule ya Msingi Nyamkazi. Akiwa ni mtoto wa tatu katika familia yenye watoto saba, Majaliwa alishindwa kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na kushindwa kumudu mahitaji ya shule. Mama yake mzazi, Arodia Bernard, mkazi wa Nyamkazi, Kata ya Miembeni anathibitisha hilo akisema, mtoto wake aliacha shule kutokana na kukosa sare.
Pia wakati mwingine, alishindwa kuhudhuria shule kutokana na kulazimika kutafuta fedha ya matumizi, jambo ambalo alikuwa akipewa adhabu kali shuleni, hali iliyomkatisha tamaa. Hata hivyo, Arodia anamwelezea mwanaye kuwa ndoto ya kusoma iliendelea kwani kilipozinduliwa chuo cha VETA mkoani Kagera, Majaliwa alianza kuweka akiba kwa ajili ya kwenda kusomea udereva. “Aliniomba nianze kumwekea akiba ya hela anayoitafuta,” anasema.
Arodia na kueleza zaidi mazingira magumu aliyopitia Majaliwa kuwa ni pamoja na kulazimika kuhudumia familia baada ya yeye (mama) kuugua kifua kikuu kwa muda mrefu. “Ndiye alilazimika kutafuta hela ya chakula kwa kufanya kazi ndogondogo mwaloni.”
“Siyo kwamba hapendi kusoma; tatizo ni uwezo… ana wadogo zake wanne wanaosoma shule ya msingi. Huyu ndiye alikuwa akinisaidia kutafuta matibabu na kuhudumia wadogo zake,” anasema Arodia ambaye amekuwa akifanya shughuli ya kuanika dagaa mwaloni na shughuli nyingine za vibarua huku akilea watoto mwenyewe. Baada ya kuacha shule, Majaliwa aliamua kutafuta riziki kwa kuanika dagaa mwaloni na kuwauza.
Majaliwa pia katika mahojiano na HabariLEO, anakiri kwamba alipenda kusoma lakini hakuweza kumudu mahitaji ya msingi. Anaweka bayana kuwa alikuwa tofauti na wenzake kwa maana ya sare alizokuwa akivaa. Baadhi ya wanafunzi waliosoma naye shule hiyo ya Rumuli wanakiri juu ya changamoto hizo za kipato zilizokuwa zikimkabili. Ni katika harakati hizo za kutafuta fedha ya kukidhi mahitaji yake na familia pia, ndipo alishuhudia ajali hiyo ya ndege ya Precision. Aliiona wakati akitafuta chenji ya mteja aliyenunua dagaa.
“Sijawahi kuwa mvuvi, kwa sababu nyumbani wanasema mimi bado ni mdogo. Lakini nimezaliwa mwaloni. Ninachojua ni kuogelea kwa maji mafupi,” anaelezea tukio hilo lililoacha taifa katika majonzi makubwa. Anasema wakati ajali inatokea, alikuwa kwenye kazi yake ya kuuza dagaa, aliona ndege ikizunguka lakini kilichomshtua ni ndege kutokea upande wa Kyaka wilayani Missenyi, wakati si kawaida.
“Na ilipokuja, ikaenda moja kwa moja kama inataka kutua kisiwani Msira…nikasimama kuangalia hii show ikoje, nikaona inageuza kama inaenda bandarini, lakini nako ikageuza kwa mwendo wa taratibu ndipo rubani akaiweka ndani ya maji.”
Alivyoongoza uokozi Kwa mujibu wa Majaliwa, wakati wa tukio hilo, kulikuwa na wavuvi wanaotoka kuvua samaki aina ya sato wakiwa na mtumbwi mdogo ambao aliwashitua kuwa kuna ajali. “Niliwaambia wenzangu kwamba hiyo ni ajali, wakasema ni maji marefu hatuwezi kufika kwa mtumbwi.
Lakini niliwaambia wanisogeze nitaogelea,” anaendelea kusimulia. Wakiwa watatu, walisukuma mitumbwi yao hadi eneo la tukio na kubaini watu ndani ya ndege wakihangaika kufungua mlango. Kijana huyu anasema hajui roho iliyomuingia na kufika kwenye ndege hiyo iliyozama, kwani marafiki zake watatu waliishia njiani. Baada ya kufika, anasema aliona watu wanapunga mkono madirishani wakiomba msaada.
Aliwaomba wenzake wamrushie kasia kwa nguvu imfikie na walifanya hivyo. Aliitumia kuvunja mlango na abiria, akawatoa baadhi na kuanza kuwapakia kwenye mtumbwi kabla ya baadaye kuhamia upande mwingine kwa ajili ya kumwokoa rubani, jambo ambalo hata hivyo halikutimia. “Mlango ulikuwa kama umejifunga… nikatumia kasia langu na kuuvunja kwa nguvu, ukafunguka na watu wakaanza kutoka.
Mimi nikahamia upande wa pili wa rubani nikazama hadi nikamuona rubani akanielekeza nipasue kioo.” Anasimulia zaidi: “Nikatoka nje ya maji, nikaomba walinzi wa uwanja wa ndege waniletee kifaa cha kuvunjia wakaniletea vishoka.” Anasema wakati anaondoka, mwanaume mmoja aliyekuwa na kipaza sauti, alimkataza kuvunja kioo kwa sababu rubani anawasiliana nao kwenye simu na maji aliko hayapo mengi.
Kulingana na maelezo ya kijana huyo, ilibidi arejee tena kuzamia hadi kwa rubani na kumpungia mkono wa ‘kwaheri’. Lakini rubani alimwonesha mlango wa dharura. Majaliwa alichukua kamba akiwa na wavuvi wenzake na kuifunga kwenye mlango huo ili wauvunje na kuokoa abiria.
Anasema kamba waliyotumia ilikuwa inavutika na walipoifunga, wakati anamalizia ili wauvute mlango huo, bahati mbaya kamba ilivutika, ikampiga usoni akapoteza fahamu na alipoamka alijikuta katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera. Katika kudhihirisha kuwa Majaliwa ni kijana anayetambulika na kuthaminiwa katika jamii, walijitokeza marafiki, wengi wakiwa wanaofanya naye shughuli mwaloni, waliokwenda kumjulia hali huku wakisisitiza kitendo chake kuwa ni cha kishujaa.
Akisisitiza kuwa hakuwa na elimu yoyote ya uokoaji, anasema licha ya kutokuwa na matarajio ya kuendelea kimasomo, aliwahi kumuomba Mungu amwezeshe kufanya kitu kikubwa cha kusaidia taifa.
Alivyookoa wavuvi Hata hivyo, Arodia ambaye ni mama yake Majaliwa, anabainisha kuwa hii si mara ya kwanza kuokoa watu katika maji kwani mwaka jana, aliwahi kuokoa watu kadhaa waliotaka kuzama majini katika eneo hilo jirani na Nyamkazi wakitoka katika Kisiwa cha Msira. “Kuna watu waliotaka kuzama na mtumbwi… alisaidia pakubwa.”
Kuhusu kusaidia watu wa kawaida waliomzunguka, anasema hiyo ni kawaida yake tangu akiwa mdogo. “Ni mwenye huruma.” Anatoa mfano wa ambavyo amekuwa akisaidia kubeba watoto (wanafunzi) wanaotoka kisiwa cha Msira wanaosoma shule ya Nyamkazi hasa kipindi cha mvua kubwa ambayo husababisha mafuriko kuanzia mwaloni hadi kwenye shule hiyo.
‘Avikwa pete’ Kama ulivyo msemo wa Kiswahili, ‘Chanda chema huvikwa pete’, Majaliwa amepongezwa kwa ushujaa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni kumtafutia nafasi kwenye Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili apate mafunzo zaidi ya uokoaji.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitangaza ‘zawadi’ hiyo juzi katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, kwenye shughuli ya kuaga miili ya watu waliofariki katika ajali hiyo. “Kwa ujasiri alioonesha kijana huyu, Mheshimiwa Rais ameagiza kijana huyu akabidhiwe kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ili apate mafunzo ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kupata mafunzo zaidi ya uokoaji,” alisema Waziri Mkuu.
Katika shughuli hiyo ya kuaga, Majaliwa alipewa pia Sh milioni 4.3 na viongozi mbalimbali kama pongezi. Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila alimkabidhi Sh milioni moja aliyoagizwa na waziri mkuu ampatie. Mbunge wa Bukoba Mjini, Steven Byabato alimpatia Sh 300,000. Kampuni ya Precision Air imetoa Sh milioni mbili kwa umoja wa vijana waliosaidia uokoaji ambao Majaliwa ni miongoni.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Kamishna Jenerali, John Masunga, imesema Majaliwa anatarajiwa kuanza mafunzo ya zimamoto na uokoaji na ya uaskari katika Chuo cha Jeshi hilo kilichopo Chogo wilayani Handeni mkoani Tanga. Mkurugenzi wa Idara ya HabariMaelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari Bukoba mkoani Kagera jana, alisema Majaliwa anatarajiwa kupata mafunzo hayo ya kijeshi kwa takribani miezi minne.
“Tumefanya ili kuonesha kujali juhudi za ujasiri wa vijana.” Huyu ndiye Majaliwa; shule, kutunza familia hadi uokoaji.