Majaliwa: Tukutane Mei 17 tuzungumze zaidi

LICHA ya kufika Kariakoo na kuzungumza machache kuhusu mgomo wa wafanyabiashara wa eneo hilo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wawakilishi wa wafanyabiashara hao kukutana nao Mei 17, 2023 katika Ukumbi wa Anatouglou kwa ajili ya mazungumzo zaidi.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Mei 15, 2023 wakati akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Kariakoo kuhusu mgomo wao uliotokana na kile walichodai kukithiri wa tozo na utitiri wa kodi.

Akiwa eneo hilo jioni hii, Majaliwa ameagiza kufutwa kwa kikosi kazi cha Mamlaka ya Mapato ( TRA ) ambacho huwa kinapita maeneo hayo kukusanya kodi ambapo amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan alishakemea uwepo wa kikosi hicho.

Advertisement

Pia Waziri Mkuu Majaliwa amekemea baadhi ya tabia za uonevu dhidi ya wafanyabiashara hao.

Sambamba na hilo, Waziri Mkuu amesema haipaswi kwa kiongozi yoyote wa juu kumdharau kiongozi mwingine aliye juu yake na chochote anachozungumza ni agizo linalostahili kutekelezwa.