WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema nchi ina kiwango cha utoshelevu wa chakula kwa asilimia 115.
Ametoa kauli hiyo leo Septemba 23, 2022 mjini Dodoma, wakati akiahirisha Mkutano wa Bunge la 12.
“Tathmini ya awali ya uzalisha mazao ya chakula imeonesha uzalishaji umefikia tani milioni 17.4, ambapo mazao ya nafaka ni tani milioni 9.4 na mazao yasiyo ya nafaka ni tani milioni 7.9, ”amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Amesema mahitaji yote ya chakula yanayojumuisha nafaka na yasiyo ya nafaka kwa mwaka 2022/2023, ni zaidi ya tani milioni 15, ambapo tani milioni 9.5 ni mazao ya nafaka na tani mlioni 5.5 ni mazao yasiyo ya nafaka.
“Kwa kulinganisha mahitaji, nchi yetu ina kiwango cha utoshelevu wa chakula kwa asilimia 115, ” amesema.
Amesema ili kuhakikisha hali ya chakula inaendelea kuimarisha, serikali imewezesha wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula kuhifadhi tani 147,142 na kuendelea kununua mazao ya chakula kwa ajili ya kuhifadhi.
“Nitumie fursa hii kutoa wito kwa wananchi kuendelea kuhifadhi akiba ya chakula tuliyonayo na kuwa na matumizi sahihi ya chakula,”amesisitiza Waziri Mkuu.