Majaliwa: Tushirikiane kutokomeza Kifua Kikuu
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wananchi waungane na serikali na wadau wa maendeleo kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) na kuzuia maambukizi mapya pamoja na vifo.
Alitoa wito huo wakati akizungumza na mamia ya wananchi na wadau waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Bariadi, mkoani Simiyu jana, sambamba na kuzindua Mkakati wa Uwajibikaji wa Pamoja wa Kisekta dhidi ya Kifua Kikuu (MAF – TB).
“Tunahitaji kuungana na kuweka mikakati ya pamoja ya kuutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu. Iwapo kila mmoja wetu atatekeleza wajibu wake, katika mapambano dhidi ya kifua kikuu, tunaweza kukata mnyororo wa maambukizi mapya na kuzuia vifo visivyo vya lazima kwa kuwa ugonjwa huu unatibika na kupona kabisa,” alisema.
Majaliwa aliongeza: “Kila mmoja wetu, ana wajibu wa kuhakikisha anachukua hatua zote za tahadhari kwani mgonjwa mmoja wa kifua kikuu ambaye hajagunduliwa na kuwekwa katika utaratibu wa matibabu, ana uwezo wa kuambukiza watu kati ya 10 mpaka 20 kwa mwaka.
“Nitoe rai kwa kila mwananchi kuzingatia maelekezo ya yanayotolewa na Wizara ya Afya na Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa katika kujilinda dhidi ya ugonjwa huu.
”
Alisema mkakati uliozinduliwa jana ni takwa la kidunia na umekuja wakati muafaka ambapo Tanzania ikiwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa inatekeleza Mkakati wa Dunia wa Kutokomeza Kifua Kikuu ifikapo mwaka 2030.
“Mkakati huu pia unaenda kuimarisha ushirikiano wa kisekta ambao kwa muda mrefu umekosekana kwa kutokuwepo kwa chombo au uratibu wa pamoja… ninazielekeza wizara zote zilizobainishwa katika mkakati huu ziweke vipaumbele vya kimkakati vya kupambana na ugonjwa huu ili kuyaokoa makundi yaliyo katika hatari ya kuugua kifua kikuu kama vile wachimbaji wa madini kutokana na uchimbaji usiozingatia njia sahihi za kujikinga na vumbi litokanalo na upasuaji, uchorongaji au usafirishaji wa udongo wenye madini,” alisema.
Alitaja sababu nyingine inayochangia kuongezeka kwa maambukizi ya kifua kikuu kuwa ni ufinyu wa hewa katika sehemu za kazi au uwepo wa makazi duni na aliziagiza halmashauri zitenge maeneo ya wazi ya wananchi kupumzikia na pia zijenge viwanja vya michezo na burudani kama njia ya kuwezesha wananchi kupata hewa safi.
Alisema kutokana na hatua zinazochukuliwa na serikali, Tanzania imepiga hatua katika kutokomeza kifua kikuu nchini.
“Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa kwa mwaka 2022, vifo vinavyosababishwa na kifua kikuu vimepungua kutoka 55,000 mwaka 2015 hadi 25,800 sawa na asilimia 55.
“Hali kadhalika, tumepunguza maambukizi mapya ya kifua kikuu kutoka wagonjwa 306 katika kila idadi ya watu 100,000 na kufikia wagonjwa 208 katika kila watu 100,000 ikiwa ni sawa na kupungua kwa asilimia 32,” alisema.
Katika hatua nyingine, Majaliwa aliwaagiza wakuu wa wilaya wahakikishe wanasimamia kwa karibu fedha za ununuzi wa dawa zinazotolewa kila mwezi ambazo ni wastani wa Sh bilioni 17 ambapo katika kipindi cha miaka miwili Sh bilioni 462 zimetumika.
“Vile vile kwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan,serikali ya awamu ya sita imeongeza aina ya dawa muhimu zinazotakiwa kupimwa kufikia aina 290 za dawa muhimu kutoka 30 za awali.
“Hatua hiyo, imeongeza upatikanaji wa dawa muhimu kutoka wastani wa asilimia 58 Juni, 2021 hadi kufikia asilimia 71, Januari, 2023,” alisema.
Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wananchi na wadau waliohudhuria maadhimisho hayo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema takwimu zinaonesha kuwa wagonjwa 71 wanapoteza maisha hapa nchini kila siku kutokana na ugonjwa huo na akawasihi wananchi wawahi tiba kwa sababu ugonjwa huo unatibika endapo mtu awahi kwenda kupata huduma.
Kuhusu uwepo wa ahueni ya tiba hiyo, Ummy alisema: “Hivi sasa dawa zinatolewa kwa miezi sita tofauti na ilivyokuwa awali ambapo tiba nzima ilikuwa ni ya miezi 18 na sasa hivi siyo lazima mgonjwa alazwe hospitali, bali pale anapoanza matibabu, atakubaliana awe anapata vipi dawa zake kwa muda wote wa miezi sita.”
Naye Mwakilishi wa Taasisi ya CDC, Dk George Ngomela alisema walio kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wachimbaji wa madini na wahudumu wa afya.
Alisema changamoto kubwa kwenye tiba ya ugonjwa huo ni usugu wa dawa za kifua kikuu na kuongeza kuwa usugu wa dawa za kifua kikuu ni tatizo kubwa kwa nchi nyingi duniani na kwa maana hiyo inatakiwa kuchukua hatua za haraka ili kudhibiti usugu wa dawa hizo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahaya Nawanda alisema mkoa huo umepokea Sh bilioni 17 za kuendeleza majengo ya hospitali, vituo vya afya na maboma ya zahanati.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea vifaa tiba vingi mkoani kwetu. Sasa hivi tuna mashine ya CT scan katika Hospitali ya Mkoa, mashine za X-ray kwenye wilaya zote tano za mkoa huu. Kwa hiyo mwananchi hana haja ya kwenda tena Mwanza, KCMC Moshi au Muhimbili bali anapanda baiskeli yake na kufika hospitalini ili apatiwe huduma,” alisema.
Kuhusu mashine za kupima Kifua kikuu, Dk Nawanda alisema wamepokea mashine nane za utambuzi ambazo zinaweza kutoa majibu ndani ya saa mbili tangu vipimo vilivyochukuliwa tofauti na zamani ambapo ilichukua siku tatu hadi saba na kuongeza kuwa kutokana na mashine hizo, wameweza kutambua wagonjwa 3,689 ambapo kati yao, asilimia 90 wametibiwa na kupona.