MAJALIWA: Wizara ya Fedha Walindeni watumiaji wa huduma za fedha

ARUSHA:Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Fedha iimarishe mifumo ya kuwalinda watumiaji wa huduma za fedha ili baadhi ya watoa huduma wasio waadilifu wasitumie changamoto ya uelewa mdogo wa masuala ya fedha kwa baadhi ya wananchi na kuwadhulumu.

Pia, Majaliwa amesema Wizara ya Fedha iendelee kushirikiana na na watoa huduma za fedha kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo muhimu yakiwemo ya usimamizi wa fedha binafsi, kuweka akiba, mikopo, uwekezaji kupitia hatifungani na hisa, bima, mpango wa kujiandaa na maisha ya uzeeni pamoja na kodi.

Advertisement

“Wizara ya Fedha iandae mpango maalumu wa kutoa hamasa kwa Watanzania ili wajenge utamaduni wa kutumia huduma rasmi za kifedha, pia elimu iendelee kutolewa kuhusu wajibu wa kila mmoja kudai na kutoa risiti kwa malipo yanayofanyika. “

Ametoa maagizo hayo leo Novemba 22, 2023 alipofungua Wiki ya Huduma ya Fedha Kitaifa, jijini Arusha, ambapo ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa watoa huduma za kifedha wapunguze gharama za upatikanaji wa huduma za fedha zikiwemo riba na ada ili wananchi wengi watumie huduma za fedha zilizo rasmi.

Pia, Waziri Majaliwa ameisisitiza Wizara ya Fedha iendelee kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Programu ya kutoa elimu ya fedha kwa umma na kuhakikisha kuwa elimu hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi mijini na vijijini.

Aidha,Waziri Mkuu amesema Wizara ya Fedha inatakiwa iandae mpango maalumu wa kutoa hamasa kwa Watanzania ili wajenge utamaduni wa kutumia huduma rasmi za kifedha pamoja na kuratibu gharama za huduma za fedha. “Pia, elimu iendelee kutolewa kuhusu wajibu wa kila mmoja kudai na kutoa risiti kwa malipo yanayofanyika.“

Waziri Mkuu amesema lengo la maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa na Maonesho ya Huduma za Fedha yamejikita katika kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya huduma za fedha zinazotolewa, kusimamia vizuri rasilimali fedha ikiwa ni pamoja na kuimarisha utamaduni wa kujiwekea akiba, kukopa kutoka vyanzo salama na njia sahihi za kulipa madeni ili kujenga uchumi na kuondoa umaskini.

Naye, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amesema Serikali inaendelea kukuza uelewa kwa Watanzania kuhusu masuala ya kifedha huku akitoa wito kwa Watanzania kuweka utaratibu wa kusoma vigezo na masharti ya huduma za kifedha wanazopata kutoka katika taasisi mbalimbali za kifedha ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza baadae.

1 comments

Comments are closed.