Majanga ya kijamii kupatiwa ufumbuzi

HUENDA baadhi ya majanga yanayoikumba jamii nchini yakapatiwa ufumbuzi baada ya wadau kuwaza namna nzuri ya kujikomboa.

Asasi ya kiraia ya Education Gauge for Growth Tanzania (EGG-Tanzania) inatarajia kuanzisha kitengo cha uokoaji kitakachoshirikiana na vitengo vya uokoaji vya serikali ili kutoa misaada wakati wa majanga mbalimbali ya kijamii nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi hiyo , Jumanne Mpinga amesema hayo Februari 25,2023 mjini Morogoro wakati  wa kongamano la tafakuri ya tetemeko la ardhi lililotokea nchini Uturuki na Syria.

Amesema kuanzishwa kitengo hicho ni kutokana na dhima kuu ya Asasi hiyo imeguswa na matukio ya ajali ya tetemeko la ardhi lililotokea nchini Uturuki na Syria , Februari 6, 2023 na kusababisha vifo vingi vya watu na  maelfu ya makazi kuteketea.

Mpinga amesema kitengo hicho kitaratibu utoaji wa elimu kwa vijana watakaokuwa tayari nchi nzima kwa kutumia wataalamu kutoka serikalini na wadau wengine waliothibitishwa na serikali.

“ Ni matumaini yetu kuwa, kupitia kitengo hicho jamii zetu zitakuwa na vijana madhubuti wenye utaalamu na ari ya kujitolea kushiriki katika uokoaji na hivyo kusaidiana na vitengo vya serikali na visivyo vya serikali kutoa misaada ya haraka pale inapohitajika” amesema Mpinga

Mkurugenzi mtendaji wa Asasi hiyo yenye makao yake makuu mjini Morogoro amesema wanaamini kuwa baada ya hadhara hiyo, jamii yetu itakuwa na mtazamo chanya juu ya ushiriki wa mtu mmoja mmoja au vikundi katika kujielimisha elimu ya kukabiliana na majanga.

Mpinga amesema kuwa dhima kuu ya Asasi hiyo  ni kuendesha kituo cha mfano cha elimu jumuishi , usaidizi wa huduma za jamii katika sekta ya elimu na ushauri wa kitaalamu kwa wadau katika kuhamasisha mapinduzi ya mfumo wa elimu nchini.

“ Tumekuwa tukishirikiana na serikali na wadau wengine katika kutatua changamoto mbalimbali zinazogusa sekta ya elimu “ amesema Mpinga

Mwakilishi wa mkuu wa wilaya ya Morogoro,  Janeth Chatta amesema majanga yapo ya aina mbalimbali na yanatokea katika jamii yetu kila uchao.

Amesema kukua kwa teknolojia ya simu na mawasiliano hasa ya mitandao ya kijamii majanga  ya ajali za magari, moto , mafuriko  na mengineyo , watu wamekuwa badala ya kuwahi kusaidia kuokoa watu wanakwenda kupiga picha na kurusha kwenye mitandao ili ionekane yeye ndio mtu wa mwanzo kurusha kwenye mitandao .

“ Hali hii inatutoa katika utu na heshima ya mwanadamu na ni  unyama usio wa kawaida  jambo ambalo halikubaliki na haliwezi kuendelea kuvumiliwa  bali liendelee kukemewa “ amesema Chatta  ambaye ni Ofisa Tawala wa wilaya hiyo.

Kwa upande wake mwakilishi wa meya wa Manispaa ya Morogoro, Diwani wa Kata ya Mafiga Mchungaji Thomas Butabile amewasihi watanzania kuendelea kuchukua tahadhari ili kukabiliana na majanga wakiwemo mafuriko kwa wale wanaoshi maeneo hatarishi .

Habari Zifananazo

Back to top button