WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameagiza kuimarishwa kwa kanzi data ya viongozi na maofisa watendaji wakuu wanawake katika sekta ya umma pamoja na sekta binafsi kwa ajili ya kupata taarifa, ambazo zitaeleza utekelezaji wa malengo endelevu.
Ametoa maagizo hayo katika taarifa yake iliyosomwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu),Patrobas Katambi katika mkutano wa 11 wa maofisa watendaji wakuu wanawake Tanzania uliofanyika jijini Dar es Salaam.
” Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Watoto na Makundi maalum kupitia idara husika iimarishe kanzi data….kama sehemu ya utekelezaji wa maandalizi ya utoaji taarifa ,” amesema.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa lengo kubwa la kufanya hivyo ni kupima shabaha na viashiria ili kupata takwimu zilizo sahihi.
Pia Waziri Mkuu Majaliwa ameagiza Bodi ya Wakurugenzi Tanzania, maofisa watendaji wakuu wanawake nchini itafute namna ya kushirikiana kwa karibu na Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), ili kubaini maeneo yenye uhitaji kwa ajili ya kuandaa programu za kujenga uwezo zaidi.
“Naagiza TNBC kama viongozi wawe wa kwanza kuwatafuta maofisa watendaji wakuu ili kuonesha umakini wa serikali kwamba tuko pamoja na ninyi,” amesema.
Pia Waziri Mkuu Majaliwa ameiagiza bodi ya wakurugenzi Tanzania, maofisa watendaji wakuu wanawake na taasisi nyingine za sekta binafsi kuangalia namna ya kujenga uwezo wa wataalam wabobezi wanawake katika masuala ya uendeshaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya kitaifa ya miundombinu.
“Hii iwe fursa kuwa kwenu wanawake mnaojitambua. Sisi kama serikali tutatengeneza mazingira,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa maofisa hao, Emma Kawawa amesema wamekutana kujengeana uwezo pamoja na kutengeneza mahusiano kati yao.