SERIKALI imebainisha azma na dhamira ya kusogeza huduma za haki karibu na wananchi kwa kujenga na kukarabati majengo ya mahakama.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul alisema hayo wakati wa kujibu swali la Mbunge wa Kishapu, Boniphace Butondo (CCM).
Butondo alitaka kujua mpango wa serikali wa kuhakikisha kila kata inakuwa na mahakama hasa maeneo ya vijijini.
Naibu waziri alisema serikali inayo azma na dhamira ya kusogeza huduma za haki karibu na wananchi, hususani kwa kujenga na kukarabati majengo ya mahakama.
“Katika kutekeleza azma hii, tunao mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya mahakama katika ngazi zote, kuanzia mahakama za Mwanzo hadi Mahakama ya Rufani,” alisema.
Alisema kwa upande wa mahakama za mwanzo, dhamira ya serikali ni kuhakikisha kila tarafa inakuwa na Mahakama ya Mwanzo.
“Baada ya kukamilisha hilo tunataka baadaye tuweze kwenda hadi ngazi ya kata kadri upatikanaji wa fedha utakavyoruhusu,” alisema.