IDADI ya vifo kutokana na ajali za barabarani imepungua kutoka vifo 1,037 mwaka jana katika kipindi cha kuanzia Januari mpaka Oktoba hadi kufikia vifo 725 mwaka huu katika kipindi kama hicho.
Pia idadi ya majeruhi imepungua kutoka 1,689 mwaka jana katika kipindi cha kuanzia Januari mpaka Oktoba hadi kufikia majeruhi 1,011 kipindi kama hicho mwaka huu Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Ramadhani Ng’anzi alisema hayo alipozungumza na HabariLEO ofisini kwake Dar es Salaam.
Kamanda Ng’anzi alisema kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu kulikuwa na ajali 1,879 ikilinganishwa na mwaka jana katika kipindi kama hicho ambapo kulikuwa na ajali 1,368, hivyo kufanya tofauti ya ajali 511 kati ya mwaka jana na mwaka huu kwa kipindi husika.
Alisema idadi ya vifo kutokana na ajali za barabarani imepungua kwa tofauti ya vifo 312 katika kipindi cha mwaka huu katika miezi ya kuanzia Januari hadi Oktoba ikilinganishwa na mwaka jana huku idadi ya majeruhi nayo ikipungua kwa majeruhi 678 kwa mwaka huu katika kipindi hicho ikilinganishwa na mwaka jana.
Kamanda Ng’anzi alisema kumbukumbu zinaonesha kuwa katika kipindi cha kuelekea mwisho wa mwaka ambako kuna sikukuu za mwisho wa mwaka ikiwemo Krismasi na Mwaka Mpya, matukio ya ajali huwa mengi, hivyo Jeshi la Polisi lina wajibu wa kuhakikisha watu wanasafiri wakiwa salama wakati wote.
Kutokana na ajali hizo za barabarani, alisema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu, madereva 132, abiria 325, waendesha pikipiki 138, waendesha baiskeli 22, watembea kwa miguu 102 na waendesha mikokoteni sita walipoteza maisha.
Sambamba na vifo, alisema katika kipindi hicho pia kulikuwa na majeruhi 1,011 wakiwamo madereva 143, abiria 597, waendesha pikipiki 147, waendesha baiskeli 19, watembea kwa miguu 101 na waendesha mikokoteni wanne kutokana na ajali za barabarani.
“Mikakati yetu ya kukabiliana na ajali za barabarani inajumuisha utoaji elimu ya usalama barabarani kwa makundi yote ya watumiaji wa barabara kupitia njia mbalimbali vikiwamo vyombo vya habari, kusimamia sheria ya usalama barabarani na kufanya oparesheni za ukamataji wa makosa hatarishi,”alisema Kamanda Ng’anzi.
Aliongeza, “Tanzania bila ajali inawezekana tukifuata sheria za usalama barabarani na sisi Jeshi la Polisi tutachukua nafasi yetu ya kufanya kazi kwa kuzingatia haki, weledi na uadilifu, na kila polisi hasa wa usalama barabarani akifanya hivyo, barabara zetu zitakuwa salama.” Alitaja sababu zinazochangia ajali kuwa ni pamoja na mwendokasi, ulevi wa madereva, matumizi ya simu wakati wa kuendesha gari, kuvuka taa nyekundu na kulipita gari la mbele bila kuchukua tahadhari.