Majeruhi wa ajali iliyoua 13 watoka hospitali

MAJERUHI wawili wa ajali ya gari aina ya Fuso iliyotokea katika eneo la Mto Njoka Kijiji cha Namatuhi Halmashauri ya Wilaya Songea mkoani Ruvuma na kusababisha vifo vya watu 13 wameruhusiwa kutoka hospitali.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma (Homso), Dk Majura Magafu amesema awali majeruhi hao walilazwa katika Kituo cha Afya Mpitimbi na baadaye walihamishiwa Hospitali ya Rufaa Songea kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi wa hali ya afya zao.

Dk Majura amewataja majeruhi hao ni Hassan Mbawala mkazi wa Lizaboni Manispaa ya Songea na Christopher Banda mkazi wa Majenga, Songea.

Kwa mujibu wa Dk Majura, majeruhi hao walifikishwa hospitalini hapo wakiwa na hali mbaya na baada ya kufanyiwa uchunguzi, Mbawala alionekana na michubuko midogo midogo sehemu mbalimbali za mwili wake ambapo alitibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Majeruhi mwingine, Christopher Banda baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu hakuwa na tatizo lolote ila alipata mshtuko baada ya ajali hiyo ambapo naye alitibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Marco Chillya alisema majeruhi wanaendelea vizuri japokuwa awali walilazwa katika kituo cha afya Mpitimbi na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma (Homso) kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Kamanda Chillya ameeleza kuwa miili ya watu wote 13 imetambuliwa na imeshakabidhiwa kwa ndugu na jamaa zao kwa ajili ya mazishi.

Mwili wa Christopher Msuya umebaki katika chumba cha kuhifadhia maiti kutokana na ndugu zake kupanga kusafiri kuelekea Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kamanda Chillya amerudia kutoa wito kwa wananchi kutopanda magari ya mizigo (malori) pindi wanapotaka kusafiri kwenda maeneo mbalimbali kwa shughuli za biashara au matembezi ya kawaida kwani usafiri huo ni hatari kwa usalama wao.

 

Habari Zifananazo

Back to top button