Majogoo watwaa Carabao kibabe

LONDON, England: USIKU wa jana umekuwa muruwa kwa mashabiki wa majogoo wa England, Liverpool FC kwa kutwaa kombe la 10 la Carabao kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Chelsea katika Uwanja wa Wembley, jijini London.

Shukrani kwa bao pekee la Mholanzi, Virgil Van Dijk dakika ya 118’ kwa pigo la kichwa dakika mbili kuelekea kutamatika dakika 120 baada ya dakika 90’ kutoka 0-0.

pharmacy

Advertisement

Kongole mlinda lango wa Liverpool, Caoimhin Kelleher kwa kuhakikisha anaondoka na hati safi ya kudhibiti vilivyo milingoti mitatu ya majogoo na kuibuka mchezaji bora wa mechi.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp ukiwa ndio msimu wake wa mwisho klabuni hapo, ameingia katika mchezo wa jana akiwa na damu changa kwa asilimia kubwa kikosini, baada ya takribani wachezaji wake tisa wa kutumainiwa kuwa benchi kwa sababu kadhaa ikiwemo majeruhi.

Likiwa ni kombe la kwanza la msimu, majogoo  waliingia katika fainali huku wakiwakosa, Mohamed Salah, Darwin Núñez, Trent Alexander-Arnold, Diogo Jota, Curtis Jones, Dominik Szoboszlai, Jöel Matip, Thiago Alcântara na Alisson Becker.

Ni fainali ya pili mutawalia, Liverpool anatwaa ndoo ya Carabao mbele ya Chelsea, baada ya kufanya hivyo Februari 27, 2022 kwa mikwaju 10 kwa 11 ya penalti.