Makalla amaliza zogo mabasi ya mikoani

Makalla amaliza zogo mabasi ya mikoani

MKUU  wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla ameagiza kuondolewa kwa katazo la mabasi ya mikoani na nje ya nchi kupakia au kushusha abiria katika vituo binafsi, badala yake ameruhusu utaratibu huo kuendelea kwa sharti la kila basi kuingia ndani ya Kituo kikuu cha Mabasi cha Magufuli.

Makalla ametoa uamuzi huo leo, wakati wa kikao cha pamoja kilichowakutanisha baadhi ya wamiliki wa mabasi hayo chini ya Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za Usafiri Ardhini (LATRA) na uongozi wa Manispaa ya Ubungo.

Hatua hiyo imetokana na agizo la Waziri wa Nchi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Innocent Bashungwa baada ya kupokea malaamiko ya baadhi ya wananchi hususani abiria kutaka katazo hilo kutenguliwa, kutokana na sababu mbalimbali.

Advertisement

Waziri Bashungwa alimtaka  Makalla kukutana pamoja na wadau hao, ili kupata ufumbuzi wa suala hilo lililozua taharuki kwa wananchi wengi katika maeneo mbalimbali, wakidai kuwa hatua hiyo ni usumbufu kwa abiria na kwamba uwepo wa stendi hizo binafsi uliwapa wengi unafuu.

Kutokana na hilo Makalla ameridhia uwepo wa vituo vitano vya binafsi, ambavyo kimsingi vimekidhi vigezo vya utoaji huduma baada ya kuhakikiwa na LATRA, huku akifungua milango kwa wamiliki wengine wanaohitaji kuwa na vituo binafsi kushirikiana na LATRA, ili wapatiwe vigezo na leseni.

Vituo vilivyobanishwa kukidhi matakwa hayo ni pamoja kituo cha kampuni ya basi ya Kilimanjaro, Dar Lux, Dar Express, ABC, pamoja na Kimbinyiko, ambapo sehemu ya vigezo vilivyotajwa na pamoja na uwepo wa sehemu ya kukaa abiria, choo, uwepo wa huduma za viburudisho na maegesho ya mabasi.

 

/* */