DAR ES SALAAM: Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, amefungua Kongamano la kukusanya maoni ya wadau kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya Sera mpya ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001.
Akifungua kongamano hilo Januari 09, 2024 jijini Dar es Salaam, amesema Tanzania ina sifa na hadhi ya kipekee duniani katika eneo la kidiplomasia.
Makamba amesisitiza umuhimu wa nchi kuwa na ushawishi mkubwa duniani ili kufanikiwa katika mambo yake.
Alielezea kuwa Sera ya Mambo ya Nje inatoa fursa ya kujipambanua jinsi nchi itakavyoendesha mambo yake na kujenga ushawishi wa kujiamulia.
Marekebisho haya yanakuja kufuatia mabadiliko duniani, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, kuibuka kwa taasisi zenye nguvu, na maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Kongamano hilo lilijumuisha viongozi wa serikali, wanasiasa, viongozi wa dini, wazee, wasomi, na makundi mbalimbali ya jamii. Naibu Waziri Mambo ya Nje, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, aliwahakikishia washiriki kuwa msimamo wa Tanzania katika mambo ya nje haujabadilika tangu enzi za Mwalimu Nyerere.