Makamba azindua kamati maboresho chuo cha Dk Salim

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, leo machi 20, 2024 amezindua Kamati ya Kupitia Majukumu na Maboresho ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dk Salim Ahmed Salim, kilichokuwa kinafahamika Chuo cha Diplomasia.

Lengo kuu la kamati hiyo ni kufanya tathmini na kuboresha kituo hicho ili kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.

Hatua hii inafuatia mapendekezo ya kamati iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuhusu tathmini ya utendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na taasisi zilizo chini yake, ikiwa ni pamoja na Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dk Salim Ahmed Salim.

Advertisement

Kituo hicho kimependekezwa kubadilishwa kuwa Taasisi ya Mafunzo ya Kitaaluma, Utafiti na Stadi za Kidiplomasia, pamoja na kuwa Kituo rejea cha fikra.

Waziri Makamba ameteua timu ndogo ya wabobezi kufanya tathmini ya kina na kuainisha maeneo yanayohitaji maboresho ili kituo kiweze kukidhi mahitaji ya wadau wake. Kamati hiyo ina jumla ya wajumbe nane ikiongozwa na Mwenyekiti Khamis Kagasheki.