WANANCHI wa Mji wa Makambako wilayani Njombe mkoani Njombe, wameshauriwa kutumia huduma za mawasiliano kujiimarisha kiuchumi ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika gulio la wiki lililofanyika katika Soko Kuu la Makambako, Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Asajile John alisema mawasiliano yamerahisisha upatikanaji wa fursa mbalimbali zikiwamo za kiuchumi.
Asajile alisema katika ulimwengu wa sasa taarifa nyingi za uboreshaji wa huduma, biashara, masoko na kilimo zinapatikana mtandaoni na kuwataka wananchi wa Makambako kutumia fursa hizo.
Alitoa mfano wa taarifa za uboreshaji kilimo, upatikanaji wa masoko ya bidhaa za kilimo na misitu pamoja na kutangaza bidhaa katika masoko ya ndani na ya kimataifa, kuwa zinapatikana mtandaoni na kuwasihi wananchi badala ya kutumia mitandao kufanya mambo yasiyo na faida, wajielekeze katika maeneo hayo ya msingi.
Huu ni mwendelezo wa kampeni ya kuelimisha umma juu ya matumizi bora na salama ya huduma za mawasiliano ijulikanayo ‘Kwea kidijitali’ inayoendeshwa na TCRA.