Makamu wa Rais atoa maagizo kudumisha utamaduni

Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango ametoa wito kwa watanzania wote hususan wasanii wa kizazi kipya, kuepuka kuiga kila tamaduni bila kuchuja wala kuzingatia maadili ya taifa.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni la Bagamoyo linalofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) mkoani Pwani. 

Amewataka wasanii wa muziki na filamu kuhakikisha wanazingatia maadili na miongozo ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) pamoja na Bodi ya Filamu Tanzania wakati wa utengenezaji wa maudhui ya kazi zao ili kuepukana na uvunjifu wa maadili unaojitokeza.

Pia, amesema Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inapaswa kushirikiana na wadau husika kuendelea kutoa elimu na kutafuta namna bora ya kutatua changamoto zote zinazohusiana na hakimiliki, hakishiriki, mirabaha na mikataba katika sekta ya Utamaduni na Sanaa kwa ujumla.

“Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii zihakikishe zinahifadhi, kutunza na kutangaza tamaduni za makabila kupitia utalii wa kiutamaduni (cultural tourism) na kutoa nafasi kwa makabila mbalimbali hapa nchini kuonesha tamaduni zake kwenye chakula, dawa za asili, mavazi, makazi pamoja na aina ya ngoma na burudani zake,” amesema.

Aidha, ameagiza kila mkoa kuweka utaratibu wake wa kuendeleza utamaduni wa mkoa huo kama sehemu ya utalii wa kiutamaduni.

Habari Zifananazo

Back to top button