Makarani wa mahakama wakumbushwa kutunza siri
MAKARANI wa Mahakama ya Tanzania wametakiwa kutunza tena kwa siri nyaraka za mashauri yanayowahusu watoto ili kuhakikisha wanamlinda na kumpatia haki zake pale anapokuwa mahakamani.
Aidha, jamii imetakiwa kuendelea kutoa taarifa kwa mamlaka husika dhidi ya ukatili wanaofanyiwa watoto ili kesi zifunguliwe mahakamani na kuhakikisha mtoto anapata haki.
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Nyigulila Mwaseba alisema hayo Dar es Salaam wakati wa semina kwa makarani na watunza kumbukumbu wa mahakama iliyoandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
Jaji Mwaseba alisema mafunzo hayo yametolewa kwa watunza kumbukumbu 16 na Naibu Msajili anayesimamia watoto na kwamba ni muhimu kwao kwa kuwa ndio hukutana na watoto hao kabla ya mahakimu na majaji.
“Kila karani au mtunza kumbukumbu ahakikishe analinda maslahi mapana ya mtoto kwa kuita shauri la mtoto kwa kuficha usiri wa mtoto, kutunza nyaraka kwa siri kwani si kila mtu anatakiwa kujua kama mtoto amefanyiwa ukatili au amefikishwa mahakamani,” alisema Jaji Mwaseba.
Msajili wa Mahakama ya Rufani, Sylivester Kainda alisema kuwa Novemba mwaka 2022, IJA kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania kupitia ufadhili wa Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF) waliandaa mwongozo wa kufundishia makarani wa mahakama namna bora ya kushughulikia mashauri ya watoto.
Alisema kuwa mafunzo hayo yamejikita katika kuhakikisha maofisa wa mahakama na wadau wa haki ya mtoto wanajengewa uwezo katika kushughulikia na kusimamia haki ya mtoto.
Mratibu wa Mafunzo ya Haki Mtoto kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Elena Gabriel alisema kuwa mafunzo hayo ni ya siku tatu yakilenga kuwajengea uwezo washiriki tajwa mbinu mbalimbali za kufundishia watunza kumbukumbu wasaidizi namna bora ya kushughulikia mashauri ya watoto.