Makinda afunguka umuhimu wa takwimu

DAR ES SALAAM: Takwimu zinawapa nguvu waandishi wa habari nafasi ya kujiamini, kuibua na kuhoji kwa sababu takwimu zipo wazi na hakuna atakayemsumbua.

Hayo yamesemwa leo Machi 13, 2024 na Kamisaa wa Sensa Anna Makinda jijini Dar es Salaam akizungumzia usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya Mwaka 2022 akizungumzia usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.

Alitolea mfano kuwa kwenye baadhi ya mikoa takwimu zilionyesha matumizi ya choo kuwa chini na kipindupindu kilivyoibuka hawakushangaa kwa sababu takwimu zilionyesha, hivyo mwandishi akiandika anaeleza hayo kwa sababu takwimu zipo.

“Huna haja ya kulalamika unanyimwa habari kwenye taasisi za serikali kwa sababu takwimu zipo ndani ya kiganja chako, wewe ni kuandika kutokana na sensa ya mwaka husika hapa kulitakiwa ijengwe hiki mbona hakipo, unafikiri kuna mtu atakufuata kwa sababu unaandika kufuatana na sensa,” amesema Makinda.

Amesema lengo la serikali ni kuona matokeo ya sensa yanawafikia wadau wote hususani wananchi ili waweze kuyatumia katika shughuli zao binafsi, ushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi ikiwemo katika kufanya maamuzi na kupanga mipango ya kufuatilia na kutathmini shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na serikali na wadau wengine katika maeneo yao wanakoishi.

Aidha, amesema baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kutangaza matokeo ya mwanzo mwaka 2022, ulitolewa mwongozo lengo lake kuu ilikuwa kutumia matumizi ya matokeo ya sensa ya mwaka 2022 kuongeza uelewa, kufanya uwazi na kupanua wigo wa matumizi ya matokeo ya sensa kwa serikali.

“Wananchi na wadau wote ili waweze kupanga mipango yao jumuishi kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi, kijamii na kimazingira kutokana na sensa iliyofanyika,” amesema Makinda na kuongeza

“Katika kuhakikisha lengo hili linatimizwa ndio maana serikali ilibainisha kuwa muongozo huu unakusudia kuyafikia makundi yote ya jamii na ni sehemu ya utekelezaji wa awamu ya tatu na ya mwisho wa utekelezaji wa sensa kama ilivyokuwa katika awamu ya pili na mwanzo,”

Amesema ni dhahiri kuwa sekta ya habari kote ulimwenguni imekuwa na mchango wa kipekee katika kuleta maendeleo ya kiuchumi, kisiasa, kijamii, kitamaduni na pia ni sehemu ya wananchi kuelewa kinachoendelea katika nchi.

Habari Zifananazo

Back to top button