KATIBU wa NEC Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda ametuma salamu kwa wateuliwa wote wakiwemo wakuu wa mikoa, mawaziri, wakurugenzi na watendaji wote wa serikali kuwa hatokuwa mvumilivu kwa atakayevurunda kwani hayupo tayari kubeba msalaba wa mtu.
Makonda ameyasema hayo leo Oktoba 26, 2023 katika mapokezi yake yaliyofanyika ofisi ndogo za CCM Lumumba jijini Dar es Salaam.
Amesema kila mmoja anapaswa kuwajibika ipasavyo kwenye nafasi aliyonayo kwa kufanya kazi kwa weledi na kwamba atakayeshindwa, yeye hatakuwa tayari kuwa msemaji wa chama ambacho watendaji wake hawawajibiki.
“Kazi ya chama ni kuwa sikio na kuwasemea wananchi, naomba nitumie fursa hii kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutuma salama kwa mawaziri wote, wakuu wa mikoa, wakiwakilishwa na wewe hapo….
wewe (Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Albert Chalamila) na watendaji wote, pale itakapobainika hamjafanya kazi yenu kikamilifu chama hakitasita kuchukua hatua,” amesema.
Amesema bahati nzuri anafahamika na watendaji wote hatakuwa tayari kuwa msemaji wa chama ambacho kimepewa dhamana na wananchi asimame hadharani kusema uongo.
“Kila kiongozi wa Serikali atabeba msalaba wake mwenyewe, sijahifadhiwa miaka mitatu kuja kusema uongo, sijateuliwa na CCM kuja kusema uongo na kauli iko wazi, uongo, fitina si sehemu ya chama nitakuwa mkweli daima,” amesema.
Amesema kiongozi yeyote atakayebainika hatendi sawa na kwamba chama kikajiridhisha, hawatachelewa kuchukua hatua, akitolea mfano kama ambavyo sheria za msikiti haziruhusu mtu kuingia na viatu na kwamba akibainika, haitamngojea Imam kuchukua hatua dhidi ya mtu huyo ndivyo atakavyofanya kwenye utawala wake.
“Tutachukua hatua bila kusubiri, kwa kiongozi yeyote atakayerudisha nyuma jitihada za chama kuendelea kuaminiwa na wananchi,” amesema.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akizungumza amesema ili CCM iendelee kuaminiwa na Watanzania, ni lazima watekeleze ilani ya chama hicho kwa kujibu kero wanazopitia wananchi.
“Nimesikiliza hotuba ya Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, aliyoyasema ni ukweli kwani ana nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya chama, na ili kiweze kuendelea kuaminiwa, ni lazima ahadi zilizotolewa kupitia ilani, zitekelezwe,”amesema
Comments are closed.