Makonda awa msemaji wa CCM
DODOMA; Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyokutana leo Oktoba 22, 2023 Mjini Dodoma, Katika Kikao chake maalum, chini ya Mwenyekiti wa CCM, DK Samia Suluhu Hassan, imemteua aliyepata kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda @baba_keagan kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi.
Makonda anachukua nafasi ya Sophia Mjema, ambaye ameteuliwa kuwa Mshauri wa Rais Masuala ya Wanawake, Watoto na Makundi Maalum.
Taarifa iliyotolewa na Idara ya Itikadi na Uenezi Taifa na kusainiwa na Mjema, inaeleza kuwa Halmashauri Kuu pia imeridhia kwa kauli moja na kuielekeza serikali kuendelea na hatua ya utiaji saini mikataba ya uendelezaji na uwekezaji wa bandari.
“Halmashauri Kuu ya CCM Taifa pia imemteua Rabia Abdallah Hamid kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), akichukua nafasi ya Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki,” imeeleza taarifa hiyo.