KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Paul Makonda anatarajiwa kufanya ziara mkoani Mtwara kuanzia Februari 10, 2024 akitokea mkoani Ruvuma.
Akizungumza leo mkoani Mtwara kuhusu ujio wa katibu huyo katika mkoa huo, Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara Juma Hassan amesema ziara hiyo ni muendelezo wa ziara zake za kichama mikoani.
Katika ziara hiyo Makonda atazungumza na wananchi wa maeneo mbalimbali mkoani humo ikiwemo Kijiji cha Mangaka kilichopo wilayani Nanyumbu.
Hata hivyo atasalimia wananchi wa Wilaya ya Masasi katika eneo la uwanja wa fisi.
Pia atafanya kikao cha Kamati ya Siasa ya Mkoa, kikao cha ndani na wazee, waasisi, viongozi wa dini, viongozi wa kimila na wakuu wa taasisi mbalimbali.
“Mwisho atafanya mkutano mkubwa wa hadhara katika viwanja vya sabasaba ndani ya manispaa ya mtwara mikindani”amesema Hassan
Katika hatua nyingine chama hicho kinatarajia kufanya sherehe ya maadhimisho ya miaka 47 tangu kuanzishwa kwake.
Sherehe hizo zitazinduliwa Februari 2, mwaka huu katika kata ya Kitangari wilayani Newala ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani humo Saidi Nyengedi.
Kilele cha maadhimisho hayo yatafanyika Februari 3, mwaka huu katika kata ya Kitama wilayani Tandahimba.
Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Mlezi wa CCM mkoa wa Mtwara Mizengo Pinda ambaye pia ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Akizungumza leo Januari 29, 2024, katibu huyo wa siasa na uenezi mkoani humo amesema maadhimisho hayo yanaenda na kauli mbiu inayosema “Miaka 47 ya CCM Kazi iendelee Shiriki Uchaguzi kwa Uadilifu”