Makonda kukutana na wabunge wa CCM
DAR ES SALAAM; KATIBU wa NEC Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amesema atakutana na wabunge wa chama hicho wampe uelekeo wa uenezi wanaotaka wa kistaarabu au wa vurugu.
Makonda ameyasema hayo leo Oktoba 26, 2023 katika hafla ya kumpokea baada ya kuteuliwa kuwa katibu wa itikadi na uenezi Oktoba 22, 2023 katika Ofisi Ndogo za chama hicho Lumumba jijini Dar e s Salaam.
Amesema: “Nimemuomba Komredi Chongolo Katibu Mkuu wetu na kiongozi wetu, nitaenda nyumbani (Mwanza), nimemuomba kibali chake nitakwenda kumuona Dk. Mwinyi (Rais wa Zanzibar), lakini pia nimemuomba kibali chake nitakwenda kukaa na viongozi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge wetu ambako ndiko siasa inapikwa, ili waniambie wanataka mwenezi wa namna gani. Mimi naweza kuwa Mwenezi wa aina yeyote. Ni uchaguzi wao.”
Amesema kuteuliwa kushika nafasi hiyo ni kwa mapenzi ya Mungu aliyemfungulia milango akiomba ampe hekima, busara na uvumilivu kukitumikia chama hicho tawala kwa uadilifu.
“Sina maneno mengi nasema asante sana kwa kuwa mtumishi wa wengi, ni matumaini yangu mlango ambao Mungu ameufungua atanipa hekima, busara na uvumilivu na kukitumikia chama kwa uadilifu, uaminifu na mafanikio makubwa ili nisimuabishe Mungu wala Rais aliyeniamini na kuniteua katika nafasi hii,” amesema Makonda.
Ametumia fursa hiyo kuwaomba watumishi wenzake wa chama hicho kumpa ushirikiano na kumshauri.
“Duniani kote watu wanaishi kwa taarifa na taarifa zinafanya uamuzi, ukiwa na chanzo kibovu utafanya uamuzi mbovu, lakini ukiwa na chanzo kizuri utafanya uamuzi sahihi wakati wote,” amesema Makonda akisisitiza kuwa ushirikiano utaifanya CCM kuendelea kuwa na mashiko kwa wananchi.