Makumbusho Oman kufanya jambo Tanzania

DSM; MAKUMBUSHO ya Taifa ya Kisultan ya Oman imekubali kufanya maboresho mbalimbali kwa Taasisi ya Makumbusho ya Taifa, lengo likiwa ni kuifanya taasisi hiyo kuwa ya kisasa zaidi katika kuhifadhi na kutunza nyaraka za kitamaduni na urithi wa Mtanzania.
Maboresho yatakayofanyika ni katika kujenga na kukarabati eneo la Makumbusho Kwa kujenga jengo la kisasa la ghorofa mbili litakalotumika kutunza na kuhifadhi utamaduni na urithi wa Mtanzania na uhifadhi wa nyaraka za dhana ya Kiswahili na muunganiko wake na Oman pamoja na historia ya wakoloni kwa nchi hizo mbili.
Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki amesema hayo Dar es Salaam wakati akifunga rasmi mkutano wa pamoja wa kiufundi kati ya Makumbusho ya Sultani ya Oman na Makumbusho ya Taifa ya Tanzania.
Hafla hiyo pia imehudhuriwa na Balozi wa Oman nchini Tanzania, Saud bin Hilal bin Saud Al Shaidhani, Katibu Mtendaji wa Makumbusho ya Sultani ya Oman, Jamal bon Hassan al-Moosawi wakiwa pia na ujumbe kutoka Oman.
Akizungumza Kairuki amesema pamoja na maeneo hayo pia Oman imekubali jengo hilo la ghorofa mbili litajengwa kwa uendelevu kwa maana kuwa iwapo siku za mbeleni itahitajika kuendeleza liweze kutekelezwa,jambo ambalo Oman walikubali.
Amesema pia Oman imekubali kusaidia mpango wa uendelezaji wa taasisi ya Makumbusho ya Tanzania na kuomba kupewa ramani kwa ajili ya uendelezaji wa eneo hilo.
Kairuki amesema katika maboresho hayo kutakuwa na wasanifu majengo wa Tanzania na Oman, ili kuwezesha kupata majengo ya kipekee yenye mandhari ya muunganiko wa Kiswahilli kati ya Oman na Tanzania .
Kairuki amesema makubaliano hayo yamefikiwa ikiwa ni baada ya Rais Samia Hassan Suluhu kutembelea Oman Juni 2022 na kushuhudia kusainiwa kwa makubaliano ya ushirikiano wa uendelezaji wa maeneo mbalimbali ya utamaduni na urithi wa Mtanzania.
” Makubaliano haya yatakuwa na manufaa kwa Makumbusho zote mbili za Tanzania na Oman ikiwemo suala la uhifadhi na utunzaji, lakini pia kuboresha kwenye kidigitali,” amesema Kairuki na kuongeza kuwa maboresho yataboresha utafiti na kuendeleza miradi.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Makumbusho ya Sultani ya Oman, Jamal, amesema utekelezaji huo utawezesha makumbusho kuhifadhi, kutunza, kufanya tafiti pamoja na kutekeleza miradi mbalimbali.