Makundi maalum 15 kutoa mawazo katiba RT

KATIBU wa Kamati ya Marekebisho ya Katiba ya Shirikisho la Riadha Nchini (RT) Wilhem Giddabuday amesema kuwa makundi maalumu 15 yanatarajia kutoa maoni na mawazo juu ya urekebishaji wa katiba hiyo ili iendane na wakati kwa maslahi ya nchi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Giddabuday kwa vyombo vya ilieleza kuwa makundi yaliyopendekezwa ni pamoja na kamati tendaji ya RT,wenyeviti na makatibu wa mikoa wanachama,Baraza la Michezo la Taifa (BMT) viongozi wa kisiasa ,viongozi wastaafu wa RT na kamisheni ya michezo.

Makundi mengine ni pamoja na kundi la wanariadha wakongwe,wanariadha wa kimataifa wanaocheza sasa,wanariadhaa wa kitaifa ,wakereketwa wa riadha,wanataaluma wa michezo,kundi mchanganyiko,kundi la wanahabari  na uwakilishi wa wajumbe wa kamati tendaji za mikoa.

Alisema kamati yake iliundwa na RT na kuanza kutekeleza majukumu yake Oktoba mwaka huu kwa kuanza shughuli zake kwa kupitia nyaraka mbalimbali ili kusaidia kutimiza wajibu wake kikamilifu.

Taarifa ya Giddabuday iliendelea kusema kuwa kamati yake inapenda kuwatangazia wadau kuwa mchakato wa marekebisho ya katiba ya RT  utafanywa na wadau na wakereketwa wa mchezo wa riadha na kazi ya kamati ni kuyaratibu maoni na kuyaunganisha kwa kuyatafsri katika muundo wa rasimu ya katiba.

Giddabuday alieleza rasimu ya katiba hiyo itawasilishwa kwa kamati ya utendaji ya RT na baadaye mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wa shirikisho hilo kwa ajili ya maamuzi.

Alisema kwa mazingatio hayo kamati inapenda kuwatangazia rasmi kuwa maoni hayo yatawasilishwa na kukusanywa mbele ya kamati yake kwa kupitia mfumo na uratibu wa njia kuu mbili moja kujaza dodoso maalumu ambalo litapatikana kwa makatibu wote wa mikoa wa shirikisho hilo na kurudisha hapo hapo na dodoso la pili kujaza dodoso kwa njia Kimtandao.

Katibu alisema kamati yake inapenda kusisitiza kuwa maoni hayo yakishakusanywa na kuratibiwa ndio yatakayotengeneza rasimu ya katiba ya shirikisho hilo hivyo kila mdau na mkereketwa wa mchezo huo anao wajibu wa kutimiza fursa hiyo muhimu kupitia mfumo na uratibu uliowekwa.

Alisema kamati itaratibu zoezi hilo la kuchukua maoni ndani ya siku 35 kuanzia desemba mosi mwaka huu hivyo kila mmoja anapaswa kujitoa kuhakikisha RT inakuwa na katiba yenye maslahi ya nchi.

Habari Zifananazo

Back to top button