Makusanyo ya kodi Geita yaimarika

MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA) mkoani Geita, imesema makusanyo ya kodi mkoani hapa yameimarika kwa asilimia 67.53 kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023, ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2021/2022.

Meneja wa TRA mkoani Geita, Hashimu Ngoda, amebainisha hayo leo, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Bombambili mjini Geita yanapofanyika maonyesho ya tano ya teknolojia ya madini.

Ngoda amefafanua kwa robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha kuanzia Julai hadi Septemba 2022, TRA Geita wamekusanya Sh bilioni 11.85 katika lengo la Sh bilioni 8.92 sawa na ufanisi wa asilimia 132.93.

Amesema huo ni ufanisi wa asilimia 67.53, ikilinganishwa na makusanyo ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/2022, ambapo TRA walikusanya Sh bilioni 7.07, kati ya lengo la Sh bilioni 8.39 sawa na ufanisi wa asilimia 84.28.

Amesema hayo ni matokeo ya elimu ya mlipa kodi pamoja na sera na mazingira rafiki ya biashara yaliyowekwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu na Watanzania wanahamasika kulipa kodi kwa hiyari.

“Tunawashukuru wadau wetu na walipa kodi wote wa Geita, kwa kulipa kodi zetu kwa hiyari, na kuchangia mapato kwa serikali, kwa hiyo Geita tunakwenda vizuri kwa makusanyo ya kodi,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button