Makusanyo ya Kodi yapo chini – Dk Mpango

DAR ES SALAAM: Serikali imesema kwa muongo mmoja toka mwaka 2010 hadi 2023 makusanyo ya kodi yamekuwa chini ya asilimia 12 ya pato la taifa, kiwango hicho ni chini ya asilimia 15 kwa nchi za Afrika.

Hayo yamesemwa leo Februari 27, 2023 na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango wakati akifungua Jukwaa la Kodi na Uwekezaji la mwaka 2024 kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema, hatua hiyo imeibua mikakati mbali mbali itakayoifikisha nchi kwenye kiwango cha kodi angalau asilmia 15 au zaidi cha pato la taifa.

Dk Mpango amesema nchi nyingi ambazo zipo kwenye kipato cha kati cha chini mfano Senegal wana asilimia 18.7, Zambia wana asilimia 16.8 Ghana 14.1 Ivory Cost asilimia 13.9 na Cameron asilimi 13.3.

“Kwa muktadha huo serikali imeandelea kufanya maboresho ya sera, mifumo ya uwekezaji,”amesema Dk Mpango

Amesema, katika kipindi kifupi cha Rais Samia Suluhu Hassan, maboresho  460 sawa na asilimia 80 yamefanyika ikiwemo kurekebisha sheria za kodi ili kutoa vivutio vya kodi kwa wawekezaji wa miradi ya kimkakati chini ya kituo cha uwekezaji TIC.

“Pili kuweka utulivu wa sera za kodi ambapo viwango vya ushuru wa bidhaa vinafanyiwa maboresho kila baada ya miaka mitatu badala ya kila mwaka, kuendelea kujenga na kuimarisha vituo jumuishi vya huduma za uwekezaji na biashara, ukijumuisha vituo 10 vya utoaji huduma mipakani,”amesema Dk Mpango

Amesema, vituo sita vimekamilika na vinafanya kazi, vilivyobaki vinaendelea na ujenzi ikiwemo kuwekewa mifumo ya Tehama.

Dk Mpango amesema pia wamefanya  mapitio na kuhuisha sera na mapitio mbali mbali ili kuweka misingi mizuri na imara ya mazingira, mashauriano na sekta binafsi kupitia Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), kutoa misamaha ya kodi kwa kiwango cha asilimia 0 kwa bidhaa za malighafi, kilimo na uvuvi, dawa za hospitali, mfumo wa dirisha moja wa kutoa huduma kwa wawekezaji na wafanyabiashara ikiwemo Nida, Brela, Uhamiaji, TIC, Kazi na Ardhi.

Pia, kuanzisha ofisi ya malalamiko ya walipa kodi kuhakikisha usuluhishi wa migogoro unaotokana na sheria unafanyika kwa haraka na kwa haki.

“Hatua hii itawezesha huduma za uwajibikaji na usimamizi kupatika kwa haraka,”amesema Dk Mpango.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button