GEA Ramadhani ni miongoni mwa vijana wanaoishi na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), ambapo alipata maambukizi kutoka kawa mama yake wakati wa kuzaliwa.
Anasema alijua ana maambukizi ya VVU akiwa na umri wa miaka 10, wakati shangazi yake alipoanza kumuelekeza namna bora ya kuishi ili kuwa na maisha mazuri.
Hivi sasa Gea ana mtoto mmoja mwenye miaka miwili, lakini hana maambukizi ya VVU.
“Siku nilipojua kuwa nina VVU sikutamani kumfanya mwingine awe na hali kama yangu, kwa hiyo nikasema nitakuwa na mtu ambaye ana hali kama yangu ili tuweze kukumbushana dawa ,kutokuwa na hofu na kuondoa unyanyapaa,”anaeleza Gea ambaye mwenza wake pia anaishi na VVU.
Anaongeza: “Kwa sababu vijana wengi wako kwenye mahusiano ambayo wenza wao hawajui hali zao, wanafanya wanakuwa katika utumiaji mbaya wa dawa, uhudhuriaji hafifu katika vituo vya afya kwa sababu ya hofu ya kupoteza mahusiano.”
Gea anasema vijana wengi hawana uthubutu wa kupima VVU kujua hali zao na pia jamii inawanyanyapaa watu wanaoishi na VVU, huku wakisahau kuwa kupata VVU ni kama ajali ambayo inaweza kumpata mtu yeyote.
Gea anawashauri vijana kuelewa kuwa maambukizi yapo wanatakiwa kuwa makini kwa sababu afya zao ni za msingi, hivyo wanapokuwa wanafanya ngono zembe hawajui hali ya wenza wao wanaweza kupata maambukizi.
HALI YA VVU KWA VIJANA
Kwa mujibu wa ripoti ya Juni, 2021 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kiwango cha maambukizi ya VVU kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi ni asilimia 4.9 (asilimia 6.3 ni wanawake na asilimia 3.4 ni wanaume).
Aidha kwa maambukizi mapya ya VVU kwa mwaka kwa watu wenye umri wa miaka 15-64 nchini ni asilimia 0.25, ambapo wanawake ni asilimia 0.34 na wanaume ni asilimia 0.17,hii ni sawa na kusema maambukizi mapya kwa watu wenye umri kati ya miaka 15-64 nchini Tanzania ni takribani watu 72,000 kwa mwaka.
Kiwango cha maambukizi ya VVU kwa watu wenye umri wa miaka 15 hadi 64 nchini ni asilimia 5.0, wanawake ni asilimia 6.5 na asilimia 3.5 kwa wanaume sawa na kusema kwa wastani watu milioni 1.4 wenye umri wa miaka 15 hadi 64 wanaishi na virusi vya UKIMWI nchini Tanzania.
Asilimia 52 ya watu wenye umri wa miaka 15 hadi 64 wanaoishi na virusi vya UKIMWI nchini Tanzania, vipimo vinaonesha kuwa kiasi cha VVU mwilini kimefubazwa, ambapo kwa wanawake ni asilimia 57.5 na wanaume ni asilimia 41.2.
NBS inaeleza kuwa asilimia 60.6 ya watu wanaoishi na VVU wenye umri wa miaka 15-64 wanajua hali zao za maambukizi ni wanawake asilimia 64.9 na wanaume asilimia 52.2.
Wanaotumia dawa kati ya watu wanaoishi na VVU wenye umri wa miaka 15-64 ambao wanajua hali zao ni asilimia 93.6, walitoa taarifa kwamba wanatumia dawa za kufubaza VVU wanawake ni asilimia 95.3 na wanaume ni asilimia 89.6.
Makundi yaliyo katika hatari ni pamoja na wasichana wenye umri kuanzia miaka 15 mpaka 25, akina mama wadogo, wafanyabishara wa ngono, wanawake waliokuwa na mahusiano yasiyo na uaminifu na waishio na wenza wenye maambukizi.
Kwa kundi la wasichana balehe wa miaka 15-24 maambukizi ya VVU yanaenea kwa kasi asilimia 2.1, ikiwa ni mara tatu zaidi ya vijana wa kiume kwa asilimia 0.6.
Ofisa Ufuatiliaji na Tathimini wa Tacaids, Nyangusi Laiser anasema asilimia 60 ya kundi balehe la vijana wa kati ya miaka 15-24 walipima na kujua hali zao kwa mwaka 2020.
Anasema kati ya waviu wapya 68,000 waliokutwa na maambukizi mapya, asilimia 28 walikuwa na umri wa miaka 15 mpaka 24 na kati ya hao asilimia 67 walikuwa wasichana balehe na wanawake vijana huku wavulana wakiwa asilimia 23.
Nyangusi anasema maambukizi mapya katika maeneo ya mjini ni asilimia 5.5, huku maeneo ya vijijini ni asilimia 4.2 na idadi ya watu wanaoishi na VVU kufikia Novemba mwaka 2021 ni milioni 1.7.
Anaeleza kuwa maambukizi mapya ya VVU kufikia mwaka 2021 yamepungua kufikia 68,000, wakati vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Ukimwi vikiwa 27,000.
Katika kitengo cha kutoa huduma kwa watu wanaoishi na VVU Hospitali ya Zakhem iliyopo Mbagala jijini Dar es Salaam, vijana kutoka miaka 15-24 wanaopata huduma ni 412 ambapo wengine waliambukizwa VVU wakati wa kuzaliwa na wengine ngono zembe.
Dk Felisia Msugura ambaye yupo katika kitengo hicho anasema licha ya kuwahudumia wagonjwa hao kazi kubwa wanayofanya ni kutoa elimu ya namna bora ya kuishi kwa waliopata maambukizi na ambao hawana maambukizi.
“Kitengo hiki sasa kinahudumia watu 7940 ambapo tunawapima na kuwapa ushauri na kuwaanzishia dawa za kufubaza VVU, tuna watoto takribani 230 ambapo asilimia 91 wameweza kufikia kiwango cha kufifisha VVU chini ya moja,”anafafanua.
Dk Msugura anatoa wito kwa wazazi ambao wanaishi na VVU wapate huduma na wawalete watoto wapate huduma wakigundulika ni rahisi kuwapa dawa na wataendelea na maisha.
VIJANA WANAFAHAMU NINI?
Ingawa kupata VVU sio mwisho wa maisha kama ilivyo kwa Fatuma ambaye anaishi na VVU kwa miaka 21 sasa na kuendelea kupata huduma Kitengo cha VVU Hospitali ya Zakhiem Mbagala, lakini bado kuna haja kubwa ya kujikinga na maambukizi.
Katika mahojiano maalum na vijana wanaoishi katika Jiji la Dar es Salaam wengine wakisoma na wengine wakifanya shughuli mbalimbalim, kila mmoja ameeleza kisababisha cha vijana hasa wa kike kuongoza kupata maambukizi.
Selemani Jongo anasema kuwa wasichana wanapenda kupata vitu wanavyovihitaji bila kuwa na kipato ambacho kinakidhi mahitaji yao, hivyo huamua kutoka kimahusiano na wanaume zaidi ya mmoja.
“Wasichana wanatapa VVU zaidi kwa sababu wanashawishika na fedha sasa utakuta wanaowapa fedha wameshaathirika na VVU hivyo wanapata.”
Farida Mwanga ambaye ni mwanafunzi anasema wasichana wengi hasa wale wanaosoma vyuo vikuu wanakuwa na maisha ya kuigana na kutamani vikubwa.
“Utakuta msichana maisha yake ni ya kawaida na anataka kuishi maisha ya wengi kwa kuiga kusuka nywele kila wiki, kula vyakula vizuri hivyo anajiingiza kwenye biashara ya ngono au mahusiano ya wanaume wengi ili apate maisha anayotaka,” anaeleza Farida.
Herman Mkazi wa Ubungo anasema katika umri huo wa miaka 15-24 wasichana wanakuwa katika hali ya matamanio ya kujaribu kila kitu.
“Mwili unahitaji ,akili inataka kujaribu sasa utakuta anajiingiza sehemu ambayo sio salama kwake,” anasema Ester Magali mkazi wa Buguruni na kuongeza:
“ Kila kitu kinasababishwa na hela wengine wanataka kusuka nywele nzuri hela hana na mwingine anataka kubadilisha madera kila wiki hela hana kwa hiyo inabidi adange hapo atawapanga wanaume hadi basi.”
Anasema licha ya tamaa ya vitu vizuri, lakini pia vijana wanafanya ngono zembe kwa kurubuniwa na hali ngumu ya maisha.
JE MFUMO WA MALEZI UNACHANGIA?
Wanasaikolojia wanasema malezi bora yana nafasi kubwa sna kumfanya kijana kuwa katika maadili mema hata atakapokuwa mkubwa.
Hata hivyo marafiki na mazingira pia yanaweza kubadilisha maisha ya kijana hasa pale umakini wake unapopungua.
Msaikolojia tiba wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,Isack Lema anasema vijana wanahitaji malezi mema tangu wakiwa watoto hadi atakapokua mzazi awe na wajibu wa kumfatilia.
Naye mmoja wa wazazi aliyejitambulisha kwa jina la Mama Mese anasema malezi mabaya na hali ngumu ya maisha inachangia vijana wa kike kujiingiza katika ngono zembe na kupata maambukizi ya VVU.
“Kuna wazazi wengi hawawajibiki kulea watoto wao katika maadili mema na wapo akinamama kabisa anamwambia mtoto wa kike nenda katafute umekua sasa, unategemea huyo msichana akikutana na mwanaume akamrubuni si inakuwa rahisi?” Anahoji.
Mratibu wa mtando wa Taifa wa wanawake wanaoishi na VVU Tanzania , Veronica Lyimo anasema sababu kubwa ni ngono zembe ambazo zinatokana na utambuzi, uelewa, malezi kutoka nyumbani.
“Kumbuka malezi yanaanza katika ngazi ya familia kama mama au baba anakosa nafasi ya kukaa na kijana kumuelimisha akikutana na vijana wenzake shuleni, vyuoni na mtaani elimu atakayopewa huko kama mzazi hujandaa elimu nzuri katika ufahamu wa kijana ni rahisi sana kuingia katika njia hatarishi ya kupata maambukizi ,”anafafanua.
Kwa mujibu wa Lyimo wazazi wengine wana hofu ya kuongea na watoto kwa habari ya kujilinda pindi wanapofikia umri wa kubalehe na hofu hiyo imefanya vijana kujikuta wakipata changamoto mbalimbali katika ngazi ya familia .
Suala lingine analolizungumzia ni wazazi kuwa na muda mwingi wa kutafuta fedha badala ya kukaa na watoto, ambao wanalelewa na wasichana wa kazi hali hiyo inafanya kijana kukosa malezi mazuri yanayoweza kumsaidia kupambanua jema na baya anapopata elimu kutoka nje.
“Hiyo ni chanzo kikubwa cha huyo kijana kupata magonjwa ,changamoto nyingine ni makundi yasiyoeleweka ,marafiki wanaopotosha hao wamechangia kwa asilimia kubwa ya vijana kupotoka na kufanya yale ambayo yanapaswa kufanywa na imesababisha kuleta changamoto kubwa katika familia,shuleni na vyuoni. “
Anasema unakuta kijana amelelewa katika misingi ya kiimani anapoenda chuoni yuko huru na kukutana na marafiki wa kila aina, ambapo atachagua ni kundi gani anatakiwa kwenda.
“Akikutana na waharibifu ataingia katika uharibifu na kuja kumtoa huko ni ngumu, hivyo basi ni jukumu letu kama jamii mtoto wa mwenzako mchukulie kama mtoto wako, umlee katika misingi imara na bora akitoka awe kijana mzuri sio bora kijana,”anasisitiza.
HATUA ZINAZOCHUKULIWA
Baraza la Taifa la Watu wanaoishi na VVU Tanzania (NACOPH)limekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watu wanaoishi na maambukizi wanapata huduma inayostahili, kama matibabu na uwezeshaji wa kiuchumi.
NACOPH pia inatoa elimu kwa jamii hasa vijana, ili waweze kuepukana na maambukizi ya VVU katika maeneo mbalimbali nchini.
Mratibu wa Mtandao wa Vijana uliopo chini ya NACOPH, Cyprian Komba anasema wanatoa elimu kwa vijana wanaoishi na VVU na wale ambao pia hawana VVU .
“Wanaoishi na VVU tunawaelimisha ni namna gani bora wanaishi na VVU na kwa wale ambao hawana tunatoa elimu ya mtindo mzuri wa maisha ya namna ya kuepukana na VVU.
Anasema wanatoa elimu kupitia miradi mbalimbali katika halmashauri na kuwajengea uwezo na vijana wanaoishi na maambukizi ya UKIMWI na pia vijana wengi.
Komba anabainisha kuwa lengo lao ni kuhakikisha wanaondoa UKIMWI ifikapo mwaka 2030 ambayo ni malengo ya Dunia.
“Tuhakikisha elimu inakwanda chini kwa watu wote wale wanaoishi na VVU na wale wasio na VVU,”anafafanua.
Lyimo anasema wanashirikiana na wadau wa maendeleo wanaounga mkono afua za Ukimiwi kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 maambukizi yanapungua au kuisha kabisa kwa makundi ya wanawake na makundi ya mabinti wa rika balehe.
“Kwasababu makundi hayo yanaonekana yanaathirika kwa kiasi kikubwa na pia ni makundi yaliyoko hatarini kupata maambukizi kutokana na hali zao,tunafanya kazi na mashirika kuhakikisha kwamba tunatoa elimu ,kuweka ustawi mzuri kwa mabinti wa rika balehe kuhakikisha anaepuka ngono zembe na kutopata maambukizi ,”anasisitiza Lyimo.
SERIKALI INAFANYA HAYA
TANZANIA imetajwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ugonjwa wa Ukimwi(UNAIDS) kufanikiwa kupunguza maambukizi ya mapya ya Virusi vya Ukimwi(VVU) ambapo takwimu zinaonesha yamepungua kutoka watu 110,000 hadi 54,000 kila mwaka.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko anasema kuwa theluthi ya maambukizi hayo mapya yanatokea kwa vijana.
“Tanzania ni moja ya nchi ambazo zinafanya vizuri katika kupunguza maambukizi mapya ya VVU na makadirio ya mwaka 2016 /2017 ni asilimia 61 tu ya watu walikuwa wanajua hali zao mpaka mwaka 2021 mwishoni ni asilimia 89.7 walikuwa wanajua hali zao”anaseama.
Pia Waziri Mkuu ,Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania imefanikiwa kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kwa asilimia 58 kutoka 130,000 mwaka 2003 hadi 54,000 mwaka 2021 kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR).
Anasema kuwa kupitia mfuko huo ambao umeleta mabadiliko makubwa katika mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi umesaidia kupunguza vifo kwa asilimia 76 kutoka 120,000 mwaka 2003 hadi 29,000 mwaka 2021.
Majaliwa anasema kuwa PEPFAR kwa sasa unasaidia zaidi ya watu milioni 1.5 wanaoishi na VVU (WAVIU) kwenye matibabu kupitia mpango wa kuokoa maisha wa ARVs, ambapo kabla ya kuanzishwa kwa mpango huo WAVIU wasiozidi 1,000 ndio walikuwa kwenye Tiba ya Kupambana na Virusi vya Ukimwi.