Malika Designer abuni mavazi kwa viongozi

DAR ES SALAAM: MBUNIFU wa mavazi nchini, Malika Rashid ‘Malika Designer’ amesema amejipanga vilivyo na sasa amebuni mavazi ambayo yanaweza kuvaliwa na viongozi wakuu wa nchi mbalimbali.

Akizungumza na HabariLEO, Malika ambaye aliwahi kushiriki Miss Tanzania mwaka 2006, amesema anatamani miongoni mwa viongozi ambao siku moja wavae mavazi hayo aliyobuni yeye awe Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wanawake Afrika kwa ngazi mbalimbali.

“Ni vazi ambalo lina hadhi na linaweza kuvaliwa na viongozi wakubwa na watu maarufu sehemu mbalimbali,” amesema.

Malika amesema amewahi kubuni mavazi ambayo yalitumiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula na aliyekuwa Naibu Waziri wa Utamaduni , Sanaa na Michezo, Juliana Shonza.

Amesema kwa sasa kuna ugumu kwenye soko la ubunifu wa mavazi hasa kwenye vitendea kazi na hivyo inawalazimu kuagiza baadhi ya vitendea kazi kutoka mataifa ya nje.

Hata hivyo amesema pamoja na changamoto hizo, soko la nje lipo hasa kwa Watanzania wanaoishi mataifa mbalimbali Afrika na baadhi ya mataifa ya Ulaya ambao wamekuwa wakishonewa na kutumiwa.

“Soko la nje lipo lakini ni kwa Watanzania wenzetu, tunawashonea na kuwatumia kuna ambao wako Burundi, Uingereza na Canada,” amesema Malika.

Habari Zifananazo

Back to top button