‘Malipo ya fidia za bima yaandikwe Kiswahili’

‘Malipo ya fidia za bima yaandikwe Kiswahili’

KAMISHNA wa Bima Dk Baghayo Saqware, ametoa agizo kwa watoa huduma za bima wote, kuandaa nyaraka za malipo ya fidia kwa waathirika wa ajali katika lugha ya Kiswahili, ili kurahisisha uelewa wa andiko hilo kwa mnufaika.

Ametoa agizo hilo leo jijini hapa katika mkutano wa kusikiliza malamiko ya wananchi na wadau wa bima kwa ujumla, ulioandaliwa na Mamlaka ya usimamizi wa bima nchini (TIRA), baada ya mmoja wa washiriki kutoa ushuhuda wa jinsi anavyohangaishwa na moja ya kampuni za bima kumlipa fidia.

“Kwa kuanzia tuanze na nyaraka ya malipo ya fidia, iandikwe kwa lugha ya Kiswahi, ili wahanga waelewe kilichomo ndani yake kufanya maamuzi stahiki,” amesema.

Advertisement

Amewataka watoa huduma hao kuzingatia kanuni na miongozo ya utoaji huduma za bima, ili huduma kwa wananchi zitolewe kwa wakati unaostahili.

“Endapo nyaraka zote mwathirika wa ajali amezikamilisha na kuziwashilisha kwa kampuni husika ya bima, fidia inapaswa kutolewa si zaidi ya siku 45,” amesema Kamishna huyo.

Akiwasilisha malalmiko yake, mtoa ushuhuda, Jakline Katona amesema ni zaidi ya miaka mitano nyuma tangu apate ajali, lakini kampuni husika imekua ikimpiga danadana, licha ya kuwasilisha kila nyaraka inayohitajika.