HAPPINES Yohana (30), mkazi wa mtaa wa CCM, mamlaka ya mji mdogo wa Katoro wilayani Geita amejifungua watoto wanne.
Akithibitisha taarifa hiyo leo, Muuguzi wa Wodi ya Wazazi Kituo cha Afya Katoro, Catherine Paul amesema mama huyo alijifungua watoto hao Desemba 7, 2022 kwa njia ya kawaida.
Amesema watoto wawili ni jinsia ya kiume na wawili ni jinsia ya kike, ambapo mtoto wa kwanza (me) alizaliwa akiwa na gramu 1.5, mtoto wa pili (ke) gramu 1.4, mtoto wa tatu (ke) gramu 1.3 na mtoto wanne (me) gramu 1.5.
Akizungumuza na waandishi wa habari katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita, Happines (mama wa watototo hao), amesema huo ulikuwa ujauzito wake wa tatu, lakini ulimshagaza kwani uzito ulikuwa mkubwa sana.

“Mimi nilibeba mimba tu, ilipofikisha miezi mitatu, mimba ikawa nzito, yaani mpaka nikawa sielewi hiki ni nini, maana mimba ikawa kubwa ndani ya miezi michache,” amesema.
Mratibu tiba wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita, Dk Pasclates Ijumba amethibitisha kupokea mama huyo na watoto wake wane, ambao wapo salama na wanahudumiwa chini ya uangalizi maalumu kitengo cha watoto njiti.
Dk Ijumba ameeleza watoto hao wataendelea kuhudumiwa hospitalini hapo kwa kipindi cha wiki tano mpaka sita na uzito wao utakapoongezeka ndipo mama ataruhusiwa kuondoka.