Mama mbaroni kuua watoto wake 2, kujeruhi wengine 2 

JESHI la Polisi mkoani Mbeya limemkamata mkazi wa Mtaa wa Ilolo, Kata ya Sinde, Shari Mwambamba (27) akituhumiwa kuua wanawe wawili na kumjeruhi mwingine na mdogo wake.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga alisema tukio hilo lilitokea juzi wakati mtuhumiwa alipowashambulia kwa panga wanawe watatu na mdogo wake.

Kuzaga aliwataja watoto waliouawa ni Neema Chembe (7) na Leonard Chembe (2) na waliojeruhiwa ni Nuru Mwambamba (23) na Emmanuel Chembe (3).

Alisema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa Novemba 20 mwaka huu mtuhumiwa akiwa nyumbani na mumewe, Evarist Chembe (45) alianza kuweweseka na kuongea vitu visivyoeleweka huku akidai amemkumbuka mdogo wake aliyejinyonga Usangu Mbarali.

Kamanda Kuzaga alisema mume wa mtuhumiwa alimuita mdogo wake (wa mtuhumiwa), Nuru Mwambamba ili aje kumchukua kumpeleka nyumbani kwao kwa ajili ya kupatiwa tiba ya asili.

Alisema mtuhumiwa alikataa kwenda kwao na ndipo akatekeleza mauaji hayo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Ilolo, Ngambi Kulaba alisema alipata taarifa za kuwepo kwa tukio lisilo la kawaida kwenye mtaa wake na alipofika alishuhudia watoto wawili wakiwa wamekufa kwa kukatwa kwa panga na watu wengine wawili wakiwa wamejeruhiwa.

Kulaba alisema wakati polisi wakiendelea na upekuzi ndani ya nyumba hiyo walimwona mtoto mwingine akiwa amejificha uvunguni mwa kitanda.

“Tulimtoa mtoto huyo aliyekuwa uvunguni tukaona bado anapumua na ndipo tukaamua na yeye akimbizwe haraka hospitalini kwa ajili ya matibabu,” alisema.

Mmoja wa majirani wa familia hiyo, Mariam Mahenge alisema wanahisi tukio hilo limetokana na migogoro ya kifamilia na kwamba amekuwa akifanya biashara na mtuhumiwa.

Habari Zifananazo

Back to top button