Mambo 10 kukabili mabadiliko tabianchi Afrika

KUTOKANA na mabadiliko ya tabianchi sasa kumekuwa na mabadiliko duniani. Yanayoshuhudiwa zaidi ni ongezeko la joto, ukame, mafuriko, kubadilika kwa misimu na mengine.

Sayansi imethibitisha Afrika inaathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na mabadiliko hayo kutokana na kuwa karibu na Mstari wa Ikweta ambao uko karibu kabisa ya jua.

Hata hivyo Afrika inazalisha asilimia nne tu ya hewa ukaa huku nchi zilizoendelea zikizalisha asilimia 96. Duniani kote asilimia 70 ya nishati inayozalishwa ni chafu. Hali hiyo imefanya kuongezeka kwa joto.

Advertisement

Mwaka 2019 lilikuwa nyuzijoto 1.1, hii ni ya juu kuliko kipindi cha kabla ya viwanda, kwa mujibu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO). ili kudhibiti ongezeko la joto lisizidi nyuzijoto 1.5, inahitajika kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kwa asilimia 7.6 kila mwaka kuanzia mwaka huu hadi mwaka wa 2030.

Kufuati hilo mataifa mbalimbali Duniani yaliungana pamoja na kukubaliana kufanya kampeni ya kupunguza ongezeko la Joto kipitia Mkataba wa Paris(Paris Agreement) ambapo kila mwaka mataifa hukutana katika mkutano wa COP.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa Masuala ya Uchumi, Dk Fadhel Kaboub, ripoti ya Benki ya Dunia inaonesha ifikapo mwaka 2050 watu milioni 105 Afrika watakimbia makazi yao na watu milioni 216 watalazimika kuhama nchi zao.

Dk Fadhel ambaye pia ni Rais wa taasisi ya kimataifa ya Ustawi Endelevu, anafafanua kuwa watu watakuwa na uhitaji mkubwa wa huduma za afya, chakula, makazi, kazi na rasilimali zingine zitahitajika endapo mabadiliko ya tabianchi yasipodhibitiwa.

Kwa upande wa Afrika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara watu milioni 86 watahama makazi yao. Afrika Kaskazini watu milioni 19, Asia Kusini watu milioni 40, Asia Mashariki na Pasifiki watu milioni 49, Amerika Kusini watu milioni 17 na Ulaya Mashariki na Asia ya Kati watu milioni tano.

“Mkutano wa COP27 uliofanyika nchini Misri, Afrika bado hakuna mafanikio na mazungumzo sasa jinsi ya kujisaidia katika upotevu huo na madhara haya kwa kutengeneza mambo yanayoweza kutusaidi kwaajili ya kesho yetu hasa katika ufadhili au fungu maalumu kwaajili ya mabadiliko ya tabianchi,”anaeleza.

 Tunawezaje kuisaidia Afrika ?

Dk Fadhel anasema ripoti ya tabianchi, nishati na malengo ya maendeleo Afrika inapendekeza kuwa Mfuko wa Maafa na Madhara kwa nchi za Afrika ni muhimu na utabadilisha kwa kiasi kikubwa muundo uliopo ambao ulichangia tatizo la hewa.

“Ili kufanikisha hili ukali unahitajika na kuwa mkali ni kuingia kwenye mzizi wa tatizo kama hatutaenda tutakuwa tunatengeneza tatizo zaidi tunahitaji kuwa wazi katika yale tunayotaka ili kukamilisha mfuko huu wa maafa na hasara la sivyo tunapoteza muda kukabilina na mabadiliko ya tabiachini.

“Ukikutana na mabadiliko ya tabianchi unatakiwa kufanya hili: namba moja ni kuacha kuweka miundombinu ya nishati chafu na nchi zilizoendelea zinazalisha zaidi nishati chafu zinatakiwa kuacha: namba mbili kuweka mipango ya haraka kutoka katika hali hiyo na hivyo ndivyo sayansi inavyosema,”anasisitiza.

Baada ya athari za mabadiliko ya tabianchi kuonekana waziwazi, Dk Fadhel anabainisha inahitajika kuwa na uhuru na utawala wa mazao hasa ya chakula, kuwa huru katika kutengeneza nishati safi na kupeleka umeme kwa watu wengi zaidi na kutumia nishati safi ya kupikia badala ya kuni na mkaa na zingine chafu.

Mbinu nyingine aliyoianisha ni kupandisha thamani ya viwanda na sera imara za kutumia rasilimali zilizopo hasa madini ambayo kila watu walioko nje ya Tanzania na Afrika, wanahitaji.

Aidha anasema kuna haja ya kupanua masoko ndani na nje ya bara kwasababu kuwa na viwanda inahitaji soko na hilo halihitaji viwango vya nchi bali viwango vya Afrika kutengeneza soko kubwa duniani.

“Hakuna nchi inaweza kufanya kazi bila chakula wala nishati ni muhimu kuzingatia nishati safi, mabadiliko ya mpangilio wa usanifu wa fedha duniani na mfumo wa biashara ya kimataifa na kuwa na sarafu moja inayounganisha Afrika ni muhimu,” anasisitiza.

Mtaalamu wa Masuala ya Mazingira, Isaack Oindo anasema mifumo ya tahadhari inahitajika mapema kukabiliana na hali ya hewa, maji na hatari zinazohusiana na mabadiliko hayo, ambazo zitakuwa za mara kwa mara na kali zaidi.

“Vikubwa vinavyohitajika ni uchunguzi wa hali ya hewa ulioboreshwa, uwepo wa maarifa na uhifadhi wa takwimu, uwezo mkubwa na ujuzi wa hali ya hewa, uwepo wa fedha zilizotengwa, utawala, sheria na mbinu za sekta mbalimbali,” anafafanua.

Pia anasema ni muhimu kuwa na taarifa za takwimu kwa ajili ya kufanya maamuzi katika sekta zilizoathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa. Fidia inahitajika Afrika Anaeleza kuwa Afrika haihusiki kwa kiasi kikubwa na athari za mabadiliko ya tabianchi lakini iko mstari wa mbele kupata athari zaidi na waliosababisha madhara lazima walipe fidia kwa hilo.

“Kwahiyo tunahitaji hili kwanza kufuta madeni pili uhamisho wa rasilimali fedha kutoka kwa nchi zilizoendelea kwasababu tangu mapinduzi ya viwanda ni kwa kiwango gani wameathiri anga na kutoa gharama za soko la kaboni wanatakiwa kuwajibika zaidi.

Anasema wengine wanaweza kuwa hawawezi kulipa moja kwa moja lakini wanaweza kuleta teknolojia, njia muhimu ambazo zinaweza kusadia Afrika kustahimili mabadiliko hayo.

“Kingine waweke mipango ya uwekezaji katika nishati safi uhakika wa chakula na miundombinu inayostahimili mabadiliko na kuweza fedha za kutosha kwaajili ya uharibufu utakaotokea,”anaeleza.

Umuhimu wa COP

Oindo anasema mkutano wa mabadiliko ya tabianchi ni muhimu kwa watu wote kwasababu ni sehemu ya kuwa pamoja na kutafuta suluhu ya mkataba wa Paris pia inasaidia kujua wako wapi na wanaenda wapi.

Anasema kutokana na mazingira magumu zaidi na uwezo mdogo wa kukabili athari kutakuwa na matokeo mbaya zaidi Afrika.

Anasema COP28 inatarajiwa kutoa hesabu ya yale yaliyofanyika baada ya mkutano uliopita ambapo hadi sasa sayansi inaonesha bado hatuko kwenye njia ya kufikia malengo ya kimataifa ya kuweka viwango vya joto chini ya sentigredi mbili.

“Matokeo ya kimataifa yatatoa muhtasari wa maendeleo katika kukabiliana na hali, kupunguza, changamoto, mazingira wezeshi na mengine mengi ,”anafafanua.

 Makala haya yamewezeshwa na MESHA na Ofisi ya Afrika ya IDRC Mashariki na Kusini

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *