Mambo matatu kuingizwa Sera ya Nje

WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imetaja mambo matatu yatakayoingizwa kwenye sera mpya ya Mambo ya Nje.

Akizungumza kwenye kikao na jumuiya ya wanadiplomasia na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao, Dar es Salaam jana, waziri January Makamba alisema kutokana na mabadiliko ya kiuchumi duniani, serikali imeona ipo haja ya kufanya mapitio ya sera hiyo iliyodumu kwa zaidi ya miaka 20 iendane na hali ya sasa.

Alitaja mambo matatu mapya kuwa ni diplomasia ya uchumi, uchumi wa buluu na mabadiliko ya tabianchi, lakini sera hiyo itaendelea kubeba misingi ya sera ya awali ikiwamo ya kuhimiza amani, mshikamano na ushirikiano wa kikanda.

Aliitaja misingi hiyo ya sera ya mwaka 2001 kuwa ni kulinda uhuru wa kujiamulia mambo yetu wenyewe, kuheshimu mipaka ya nchi na uhuru wa kisiasa, kulinda uhuru, haki za binadamu, na usawa na demokrasia.

Mingine ni kuimarisha ujirani mwema, kuendeleza sera ya kutofungamana na upande wowote; kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuunga mkono Umoja wa Mataifa (UN) na jitihada za kuimarisha maendeleo ya uchumi wa kimataifa, amani na usalama.

“Tutaendelea kushirikiana na kukuza mahusiano yetu, hivi sasa tunapitia upya sera yetu ya Mambo ya Nje ili iendane na mabadiliko na mahitaji ya dunia ya leo, lakini hatutaacha kubeba misingi ya awali ya sera hii, tutaenda nayo,” alisema January.

Alisema Tanzania inazungumzia diplomasia ya uchumi ambayo ndani yake ina vitu vingi na tayari imeanza kuleta manufaa ya kiuchumi hivyo lazima pia sera ibainishe hayo ili kuwa na mwongozo katika utekelezaji.

January alisema sera ya mwaka 2001 ilieleza azma ya serikali kukuza uchumi na maendeleo ya taifa kupitia uhusiano wa kimataifa huku msisitizo ukielekezwa katika diplomasia ya uchumi.

Alisema jitihada za serikali zilielekezwa katika kuongeza wigo wa biashara ya kimataifa kupitia utafutaji wa masoko ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi, kuvutia uwekezaji wa mitaji na teknolojia kutoka nje katika sekta za kijamii na kiuchumi.

Aidha, sera hiyo ilisisitiza kutangaza vivutio vya utalii, kuongeza fursa za ajira na masomo kwa Watanzania nje ya nchi na kushawishi upatikanaji wa misaada na mikopo ya masharti nafuu kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.

Alisema manufaa ya kiuchumi yaliyopatikana na Tanzania kimataifa ni mengi yakiwamo kukuza uhusiano baina ya mataifa mengine kupitia uwepo wa mikataba na makubaliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali.

January alisema Tanzania imeboresha mazingira ya kufanya biashara, uwekezaji na uhusiano mambo ambayo yanaendelea kuifanya nchi kuongeza ushirikiano na mataifa mengine duniani.

Aidha, alisema kupitia falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya 4R (Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga upya nchi), Tanzania imefanya mageuzi kwenye siasa na kufungua ukurasa mpya wa siasa.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x