Mambo mazuri maji Gairo

WANANCHI zaidi ya 6,000  wa Vijiji vya Ngiloli, Tabu Hoteli na Ibuti, Kata ya Chigela, Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, wanapata huduma  ya maji safi na salama na kuondokana na magonjwa ya mlipuko,  baada ya upanuzi wa miundombinu ya maji maeneo ya vijijini.

Meneja wa Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya  Gairo, Mhandisi Isaac Gilbert amesema hayo katika taarifa yake kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 Kitaifa, Abdalla Shaib Kaim ,wakati wa uzinduzi wa mradi  huo.

Aesema mradi wa upanuzi wa miundombinu ya maji Vijiji vya Ngiloli, Ibuti na Tabu Hotel ulianza kutekelezwa  Oktoba, 2020 kwa fedha za programu ya PbR- Lipa kwa matokeo na unatarajiwa kukamilika Desemba, 2023 na kwamba hadi sasa mradi umefikia asilimia 85.

“ Mradi huu umewawezesha wananchi 6,045 wa Vijiji vya Ngiloli, Tabu Hoteli na Ibuti kupata huduma ya maji safi na salama na ya kutosha na  hivyo kuondokana na magonjwa ya mlipuko,” amesema Mhandisi Gilbert

Amesema  mradi huo umejumuisha ujenzi wa tanki kubwa la maji, uwekaji wa uzio eneo la tanki na uwekaji wa mabomba ya kusambaza maji kilometa 10.1.

Ametaja kazi nyingine ni uunganishaji wa vituo vya kuchotea maji 15  kwa kila kijiji  vituo vitano,  kupima wingi wa maji, kuunda chombo cha Jumuiya ya watumia maji na kukikabidhi mradi kwa ajili ya uendeshaji.

“ Upatikanaji wa maji ya kutosha na kwa muda wote kutaongeza kipato kwa jamii kwani mradi utasaidia kuongeza muda wa kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii, baada ya wananchi kuondokana na changamoto ya kutumia muda mwingi kutafuta huduma ya maji,” amesema Mhandisi Gilbert.

Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2023  Kitaifa, Kaim, amewataka viongozi ambao  wanasimamia miradi  ya maendeleo kutanguliza uzalendo kwanza na kusimamia miradi inayotekelezwa na kuhakikisha inakuwa kwenye ubora unaokubalika.

Ameridhishwa na  utekelezaji wa mradi wa upanuzi  miundombinu ya maji pamoja na matumizi ya fedha.

“Niwapongeza  ndugu zangu wa Ruwasa kwa kazi kubwa na nzuri inayoifanyika  ya kuhakikisha wananchi waishio vijijni wanapata maji safi na salama na kumtua ndogo mama kichwani ,” amesema Kaim.

Habari Zifananazo

Back to top button