Mambo mazuri miradi ya maji Katavi

KIASI cha Sh bilioni 27.7 kimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 40 ya maji mkoani Katavi katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko wakati akikabidhi mitambo ya uchimbaji visima kwa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa huo.

RC Mrindoko amesema hadi sasa miradi 15 imekamilika na tayari wananchi wanapata huduma, huku miradi 25 ikiwa hatua ya ukamilishaji.

Amewataka wananchi mkoani Katavi kuvitunza vyanzo vya maji sanjari na kuitunza miradi ya maji inayotekelezwa katika mkoa huo, ili iwanufaishe kwa kuondokana na kero ya maji.

Amesema, hakutakuwa na maana serikali kutoa mabilioni hayo ya fedha na mitambo kama vyanzo vya maji havitatunzwa.

“Niwaombe wananchi wa Katavi, tunapokuambia ondoka kwenye chanzo cha maji, ondoka kwenye msitu ambao tunautegemea fanya hivyo bila kujiuliza mara mbili,”amesema Mrindoko.

Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Mkoa wa Katavi, Mhandisi Peter Ngunula amesema, ujio wa mitambo hiyo itaongeza kasi ya usambazaji maji mkoani humo.

Ameongeza kuwa, kabla ya kufika mwaka 2025 kutakuwa na uhakika wa upatikanaji wa maji kwa zaidi ya asilimia 85, kwani mitambo hiyo ina uwezo wa kuchimba kisima hadi cha urefu wa mita 400, tofauti na awali walipolazimika kuchimba kisima cha urefu kama huo kwa kutumia mtambo zaidi ya mmoja.

Habari Zifananazo

Back to top button