WIZARA ya Maliasili na Utalii inatarajia kupata dola Bilioni 20 baada ya mazungumzo kuanza kufanyika kati yake na kampuni 22 kwa ajili ya biashara ya hewa ukaa.
Akizungumza katika Mkutano wa fursa zilizopo katika mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo biashara ya hewa ukaa leo jijini Dar es Salaam,Waziri wa Maliasili na Utalii, Angela Kairuki amesema serikali ina misitu ambayo inasimamiwa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), kuna mamlaka ya hifadhi ya Misitu na Mamlaka ya wanyamapori (TAWA).
Amesema kupitia taasisi hizo wnaweza kupata fedha zinazoweza kusaidia katika ulinzi, uhifadhi na shughuli za maliasili na utalii.
“Ni fursa kwetu na sasa tupo katika hatua ya mashauriano na kampuni hizo na makubaliano yapo hatua mbalimbali kama yakifanikiwa tunaweza kupa dola bilioni 20 kama wizara na taasisi zake,”amesisitiza.
Kwa upande wa mafanikio ya soko la hewa ukaa, amesema vijiji nane vya Wilaya ya Tanganyika iliyoko mkoani Katavi kwa kipindi cha baada ya miaka sita hadi saba wamenufaika kupata Sh bilioni nane ambayo imesaidia kujenga huduma za kijamii.
“Wameweza kutumia mapato yao kujenga vituo vya afya, kujenga ofisi za vijiji na kata,wamepata bima za afya,wamejenga shule pamoja na miundombinu nyingine na huduma za kijamii,” amesema.
Kairuki amebainisha kuwa wanachukua hatua kuhakikisha wanatekeleza afua mbalimbali kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ambapo maliasili wanaingia kwa upande wa misitu ikiwemo uhifadhi na kupanda miti.
“Tumeanza na tunashukuru sasa watu wanapanda miti kadiri unavyopanda unapunguza hewa ukaa na wanapima na wanalipwa na pia nashukuru kwa mkutano huu wa kaboni Tanzania unaendelea kujenga uelewa kwa Watanzania kuna wamiliki wa misitu,halamshauri, misitu ya kijamii na binafsi au mtu mmoja mmoja na wizara tunasimamia,”ameeleza Kairuki.
Amesema biashara hiyi ni mpya na inaweza kuwa ya muda mfupi ni vyema kutumia fursa hiyo huku akitoa angalizo kwa Watanzania watakaopata fursa washirikishe taasisi za serikali kujua hatua gani wachukue kufanikisha mikataba hiyo kuhakikisha inalinda maslahi ya taifa na inakuwa na maslahi kwao.