SERIKARI inatarajia kuboresha kanzidata ya wakulima wa zao la korosho nchini, ili kuweka taarifa sahihi za wakulima hao na kufikia lengo la kuzalisha tani 700, 000 za Korosho ghafi ifikapo mwaka 2025/26.
Kanzidata hiyo itasaidia serikali kupanga mipango yake mbalimbali ya uendeshaji wa zao hilo, ikiwa ni pamoja na ununuzi na usambazaji wa pembejeo, ugawaji wa mbegu na miche bora ya korosho, lakini pia vifungashio (Magunia), huduma za ugani, ubanguaji pamoja na utafiti wa masoko.
Akizungumza leo mkoani Mtwara, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred amesema Bodi hiyo kwa kushirikiana na mamlaka za serikali ngazi ya mikoa, wilaya itatumia mfumo wa kielektroniki wa kusajili wakulima walioandaliwa na wizara husika katika uhuishaji wa kanzidata ya wakulima wa zao hilo nchini.
Tukio hilo la uhuishaji litafanyika katika awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza itahusisha Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani na Tanga lakini awamu ya pili itafanyika katika mikoa mipya inayolima zao hilo.
Amesema, uhuishaji huo utatumia vitabu pamoja na simu janja, ambazo zimeunganishwa na mfumo maalumu wa usajili wenye uwezo wa kuchukua alama za vidole, kupima ukubwa wa shamba pamoja na idadi ya mikorosho.
“Kila Mkulima atahitajika kuhuisha taarifa zake, akiwa shambani na hili litafanyika ngazi ya kijiji na kusimamiwa na mamlaka za serikali za mitaa, hivyo wakulima wote wawe tayari kutoa ushirikiano, ili kukamilisha zoezi la usajili kwa ufanisi, “amesema Alfred.
“Kila Mkulima wa Korosho atapaswa kuhakikisha kuwa anasajiliwa, Mkulima ambaye hatosajiliwa hatopatiwa Pembejeo katika msimu ujao”,