DAR ES SALAAM: Mtihani wa darasa la saba mwaka huu umemalizika salama kwa kuwa hakuna tukio la udanganyifu lililoripotiwa.
Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Maulid amesema hayo alipozungumza na HabariLeo kuhusu mtihani huo ambao ulianza Septemba 13 na kumalizika Septemba 14.
“Ninashukuru kwa siku mbili hizi za mtihani kwa watahiniwa na wasimamizi hakukuwa na udanganyifu wa aina yoyote ulioripotiwa hapa mkoani,” amesema.
Amewashukuru wazazi, walezi, waalimu pamoja na wanafunzi waliohitimu kwa ushirikiano waliouonyesha katika mtihani huo.
Amesema wanafunzi 95,224 mkoani Dar es Salaam wamefanya mtihani huo, kati ya hapo 171 walikuwa ni wenye mahitaji maalum.
“Tunashukuru na hawa wenye mahitaji maalum wamepata haki yao ya kushiriki kufanya mtihani huu wa kumaliza,” amesema.
Jumanne ya wiki hii Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk Said Mohamed aliwataka wahusika kuzingatia sheria na kujiepusha na vitendo vya udanganyifu.
Amesema watahiniwa waliotarajiwa kufanya mitihani ya kuhitimu darasa la saba kwa mwaka huu 2023 ni 1,397,370 kwa nchi nzima.
Kati ya watahiniwa hao, 654,652 ni wavulana sawa na asilimia 46.85 na wasichana ni 742,718 sawa na asilimia 53.15.
Kwa upande wa wanafunzi waliozungumza na HabariLeo wameeleza furaha ya kuhitimu masomo hayo na kueleza kuwa bado wana safari ndefu ya kuanza kidato cha kwanza hadi chuo kikuu.
Comments are closed.