WIZARA ya Utamaduni Sanaa na Michezo, imepatiwa eneo la ekari 12 na Shirika la Nyumba (NHC) kwa ajili ya kujenga ukumbi wa Kimataifa wa kisasa wa Michezo (Sports Arena).
Akizungumza na wanahabari mara baada ya kukabidhiwa, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa leo Februai 14, 2023, amesema eneo hilo ambalo lipo Kawe, Dar es Salaam litakabidhiwa kwa mkandarasi na ujenzi utachukua muda wa miezi nane hadi kumi kukamilika.
Amesema ukumbi huo utakaokuwa na uwezo wa kubeba zaidi ya watu 16,000 unatarajiwa kuwa miongoni mwa Arena kubwa Afrika na kwamba kwa sasa Sports Arena kubwa ipo nchini Senegal, ambayo ina uwezo wa kubeba watu 15,000.
“Arena yetu itachukua watu 16,000 na tunategemea pia ichukue watu hadi 20,000 ili Watanzania wapate nafasi kushuhudia matamasha mengi katika ukumbi huo,” alisema waziri.
Ameeleza kuwa dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha sekta ya burudani na michezo zinakuwa sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa na wananchi wananufaika nazo.