IRINGA; Kwa kadri shauku inavyoongezeka, msisimko unavyozidi na tarehe inavyokaribia, maandalizi ya mbio za mwendo pole na haraka za Great Ruaha Marathon (GRUMA) zitakazofanyika Julai 6, mwaka huu ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha yameanza kupamba moto.
Wakati wanariadha kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni wakijiandaa kushiriki katika tukio hilo la hadhi kubwa linalofanyika kwa mara ya tatu katika hifadhi hiyo tangu kuanzishwa kwake; waandaaji taasisi ya SYDP, wamesema hawachoki kutumia uzoefu wao ili matarajio yao yafike lengo.
Maandalizi ya mbio hizo zinazolenga kuhamasisha utalii wa kusini, kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji na kuhamasisha jamii ya kitanzania kushiriki michezo ili kulinda afya zao, yalizinduliwa jana kwa kuonesha medali zitakazotolewa kwa washindi na vifaa rasmi vitakavyotumika kukimbilia.
Mratibu wa mbio hizo za kilometa tano, 10 na 25, Amim Kilahama amesema uzinduzi huo umefungua rasmi pazia kwa washiriki kuanza kujiandikisha kupitia tovuti ya shirika lao na vituo vitakavyowekwa katika mikoa ya Iringa, Dar es Salaam na mingineyo.
Kilahama amewaomba wadau wa utalii na uhifadhi ikiwemo wizara husika, Ofisi ya Maji Bonde la Rufiji, na wawekezaji wa sekta hiyo kujitokeza kudhamini mbio hizo zinazotarajia kushirikisha wakimbiaji zaidi ya 1,000 .
“Kama mtakumbuka mwaka jana tulikuwa na washiriki zaidi ya 200 wakiwemo waliotoka Ujerumani, Japan, China na Australia; mwaka huu tunatarajia kupata washiriki wengi zaidi kutoka mataifa ya kigeni,” amesema.
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambao ni waratibu wenza wa mbio hizo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Godwell Ole Meing’ataki amesema wanaitumia GRUMA kuthibitisha namna inavyochochea uhifadhi na kukuza utalii kwa kuvutia washiriki na mashabiki kutoka maeneo mbalimbali.
“Mbio hizi zimekuwa zikivutia watu kusafiri kuja hifadhini na kushiriki, kushuhudia na kufanya utalii, hivyo kuchochea utalii na kuleta faida kwa nchi na jamii inayozunguka hifadhi hii ya pili kwa ukubwa nchini,” amesema.