Mambo yaiva ujenzi daraja Jangwani

DODOMA; Utekelezaji wa ujenzi wa Daraja la Jangwani jijini Dar es Salaam lenye urefu wa mita 390 unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2024/25.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara yake kwa mwaka wa fedha 2024/25 bungeni mjini Dodoma leo, amesema: “Wizara imepanga kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara na madaraja katika mwaka wa fedha 2024/25.

“Mheshimiwa Spika, pamoja na miradi hiyo, Wizara kupitia TANROADS itaanza utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa ujenzi wa Daraja la Jangwani, ambao ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maendelezo ya Bonde la Mto Msimbazi.

“Daraja litakalojengwa lina urefu wa mita 390 pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa mita 710 na kina cha mita 15.5 kutoka usawa wa bahari.

“Daraja hili litakapokamilika litatatua changamoto ya kujaa kwa maji katika barabara ya Morogoro eneo la Jangwani wakati wa mvua na kusababisha kufungwa kwa barabara hiyo mara kwa mara. Tathmini ya zabuni ili kumpata Mkandarasi na Mhandisi Mshauri zinaendelea,” amesema Waziri Bashungwa.

Habari Zifananazo

Back to top button