Mambo yaiva ziara Makamu wa Biden
WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris anatarajiwa kuwasili Dar es Salaam kesho.
Waziri wa wizara hiyo, Dk Stergomena Tax amesema jijini hapa kuwa ziara hiyo ni ya kihistoria kwa sababu Harris ni mwanamke wa kwanza katika historia ya Marekani kuwa Makamu wa Rais nchini humo.
“Lakini pia anatembelea Tanzania ambayo ni nchi ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki kuwa na Rais mwanamke ambaye ni Mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Dk Tax wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari.
Alisema Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tatu katika Bara la Afrika zinazotembelewa na kiongozi huyu Mkuu wa Marekani tangu utawala wa Rais Joe Biden uingie madarakani ni uthibitisho wa uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Marekani na matokeo ya juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kukuza na kuimarisha diplomasia na ushirikiano wa kimataifa.
“Ziara hii muhimu pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani hususani kwenye maeneo ya kimkakati kama vile biashara, uwekezaji, utalii, elimu, afya na utunzaji mazingira,” alisema Dk Tax.
Alisema Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango anatarajiwa kumpokea Harris kesho katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na keshokutwa, Rais Samia atampokea Ikulu, jijini Dar es Salaam.
“Siku hiyo hiyo, Mheshimiwa Kamala Harris ataweka shada la maua katika Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam ikiwa ni ishara ya kuwakumbuka waathirika wa mabomu yaliyolipuliwa kwenye Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam mwaka 1998.
“Pia atatembelea Taasisi ya Tanzania Startup Association ya jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukutana na wajasiriamali vijana.
“Mheshimiwa Kamala Devi Harris, vilevile, atashiriki futari iliyoandaliwa kwa heshima yake na mwenyeji wake Mheshimiwa Dk Rais Samia Ikulu, jijini Dar es Salaam,” alisema Dk Tax.
Alisema Marekani ni moja ya nchi inayochangia kwa kiasi kikubwa uwekezaji nchini kwa kuwa na miradi 266 iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 4,778.6.
Dk Tax amesema sekta ya utalii inaongoza kwa uwekezaji wa Marekani nchini kwa jumla ya miradi 68, ikifuatiwa na sekta ya uzalishaji viwandani yenye miradi 66.
“Miradi hii imetengeneza ajira zipatazo 54,584 kwa Watanzania,” alisema na akaomba wakazi wa Dar es Salaam wajitokeze kwa wingi kumpokea Harris.