Mambo yaliyoitikisa Tanzania 2022

KESHO Jumamosi Desemba 31, ndio mwisho wa uhai wa Mwaka 2022. Mwaka 2022 ‘utakufa’ rasmi na kuzaliwa ‘mdogo wake’ aitwaye Mwaka 2023. Hii ni kusema kuwa, keshokutwa Jumapili, ndio Mei Mosi, 2023; Sikukuu ya Mwaka Mpya.

Mwaka 2022 unaondoka ukiwa umeacha machozi ya vilio na machozi ya vicheko na nderemo. Mwaka 2023 unaondoka; saa unakuja mwaka 2023.

MACHOZI YA VICHEKO

 Sensa ya Watu na Makazi

Miongoni mwa matukio makubwa yaliyotikisa masikio ya dunia kutoka Tanzania, ni tukio la kihistoria la Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika Tanzania nzima Agosti 23, 2022 chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na kufanikiwa kwelikweli.

Hii ilikuwa Sensa ya Tano ikitanguliwa na zilizofanyika katika miaka ya 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.

Chapisho la Matokeo ya Mwanzo katika mtiririko wa machapisho yaliyopangwa kutolewa kutokana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, linaonesha kuwa Tanzania kuna watu 61,741,120 wakiwa ni wanawake 3 1,687,990 sawa na asilimia 51.3 na wanaume 30,053,130 sawa na asilimia 48.7.

Kuhusu sense iliyotangulia, wakati akitangaza matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 mkoani Dar es Salaam, Rais Jakaya Kikwete (sasa amestaafu), alisema Tanzania Bara kuna watu milioni 43,625,434 wakati Zanzibar kuna watu milioni 1,303,568, hivyo kuwa na watu milioni 44,929,002.

Kwa mara ya kwanza sensa ya mwaka huu iliyofanyika chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia, ilifanyika kwa kutumia teknolojioa ya habari na mawasiliano (Tehama).

Sensa ya mwaka huu ilikuwa tofauti na sensa zilizopita kwani sensa za miaka ya nyuma, makarani walilazimika kubeba takwimu kuzipeleka vituoni na hivyo, kutumia muda mwingi katika ukusanyaji wa data za pamoja.

Wamaasai kutoka Ngorongoro kwa hiari kwenda Msomera

Mwaka huu dunia imeshuhudia watu wa jamii ya Kimaasai wakihama kwa hiari yao kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro kwenda Msomera wilayani Handeni, Tanga ili kupisha uendelevu na ustawi wa hifadhi hiyo ambayo ni kivutio cha utalii nchini.

Kwa miaka mingi kumekuwa na ongezeko la mwingiliano wa shughuli za kibanadamu unaoathiri vibaya uhifadhi na hivyo, Watanzania hao kuamua kuonesha uzalendo wao.

Wamaasai wameishi katika Hifadhi ya Ngorongoro, eneo la Urithi wa Dunia wa Unesco, Kaskazini mwa Tanzania, kwa zaidi ya karne moja, wakiishi pamoja na pundamilia, tembo, nyumbu na wanyamapori wengine katika hifadhi hii.

Kuongezeka kwao hifadhini kulikuwa tishio kwa makazi ya wanyamapori uhifadhi na utalii kwa ujumla.

Akiwaaga wakazi wa Ngorongoro waliohama kwa hiari kwenda Kijijini Msomera kupisha shughuli za uhifadhi, Juni 23, 2022 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema wataendelea na ufugaji wao katika mazingira bora zaidi na yenye tija.

Hiyo ilikuwa awamu ya pili ya wakazi wanaohama katika eneo hilo kuelekea Msomera.

Alisema uamuzi walioufanya wa kuhamia Msomera na kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo la Ngorongoro ni uamuzi sahihi na wa kizalendo

Mbali na kupewa nyumba za kisasa na zenye miundombinu ya kisasa, fidia na mashamba kaya zote pia zilipewa magunia mawili ya mahindi kwa kwa kipindi cha miezi mitatu ili kujikimu katika kipindi cha mpito wakati zikijiandaa na msimu wa kilimo.

Filamu ya The Royal Tour na utalii

Mwaka huu Rais Samia, akiwa New York, Marekani, Aprili 19, 2022, katika Ukumbi wa Makumbusho: Solomon R. Guggenhein, akaituliza dunia kupitia uzinduzi wa filamu ya The Royal Tour inayolenga kuitangaza Tanzania na vitutio vyake  lukuki vya utalii na uwekezaji.

Katika filamu hii Rais Samia ndiye kiongozi wa kutoa maelezo kuhusu vivutio hivyo kwa Peter Grenberg, ambaye ni mwanahabari nguli na mtozi wa filamu kutoka kituo cha televisheni cha CNBC cha Marekani.

 

Filamu ya The Royal Tour.

Samia, Dk Mwinyi, Kinana wachaguliwa CCM

Baada ya miaka mitano kupita, Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka huu kimefanya uchaguzi mkuu kuanzia ngazi ya shina hadi taifa.

Mkutano Mkuu wa 10 wa CCM wa  Desemba 2022, ulimchagua Rais Samia kwa kura 1,914 kati ya 1,915, kuwa Mwenyekiti wa CCM kwa miaka mitano, kuanzia 2022 hadi 2027.

Mwenyekiti wa muda katika mkutano huo, Dk Mohammed Ali Shein, pia alimtangaza Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dk Hussein Ali Mwinyi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar baada ya kupata kura 1,912 kati ya 1,915 zilizopigwa.

Dk Mwinyi amechukua nafasi ya Dk Shein ambaye amemaliza muda wake huku Makamu Mwenyekiti wa CCM –Tanzania Bara, Abdurahman Kinana akitangazwa baada ya kupata kura 1,913 kati ya 1,915. Kinana alipata kura za hapana mbili.

Rais Samia atunukiwa Shahada ya Udaktari

Novemba 30, 2022, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kikamtunu Shahada ya Juu ya Udaktari wa Heshima kutokana na mabadiliko makubwa ya maendeleo aliyoyafanya kwa Watanzania tangu alipoingia madarakani Machi 2021.

Katika Mahafali ya 52 ya UDSM yaliyofanyika Dar es Salaam, Mkuu wa UDSM, Dk Jakaya Kikwete anamtunuku heshima hiyo.

Baada ya kutunukiwa shahada hiyo, Rais Samia akaushukuru uongozi wa UDSM kwa kutambua na kuona mchango wake kwa Tanzania huku akikiri kujaribu kuitafuta shahada hiyo, ingawa hakufanikiwa kutokana na muda kutompa nafasi.

 

Maazimio ya Senenti ya Baraza la UDSM katika Kikao cha 875 yalimpendekeza Rais Samia kutunukiwa shahada hiyo kutokana na mabadiliko na mafanikio makubwa yaliyoletwa na uongozi wake kwa taifa.

Kujaza maji Bwawa la Julius Nyerere

Desemba 22, 2022 Tanzania, Afrika na dunia kwa ujumla ikamshuhudia Rais Samia akizindua shughuli ya kujaza maji katika Bwawa la Mradi wa Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) katika Mto Rufiji.

Kukamilika kwa mradi huu mkubwa utakaozalisha umeme wa megawati 2,115, kutaiwezesha Tanzania kuwa na umeme wa uhakika na kuchangia katika pato la taifa.

Samia alibonyeza kitufe kilichofunga handaki la kuchepusha maji, hivyo kuruhusu maji kuanza kuingia kwenye bwawa hilo lenye ujazo wa lita bilioni 33, urefu kilomita 100 na upana takriban kilomita 27.

Ukubwa wa kilomita za mraba 2,500 uliashiria hatua kubwa zaidi ya kuelekea kukamilika kwa mradi huo mkubwa utakaogharimu  takriban Sh trilioni 6.5 za Tanzania.

MACHOZI YA VILIO

Hata hivyo, Mwaka 2022 haukuwaacha Watanzania wakicheka tu, bali pia uliwapa vipindi vigumu kupitia matukio ya simanzi kama vifo vitokanavyo na matukio mbalimbali yakiwamo ya ajali za moto, ajali za barabarani na mauaji miongoni mwa wanandoa na wanafamilia.

Matukio ya ajali

Yapo matukio mengi yaliyowatoa machozi Watanzania, lakini makubwa ninayokumbuka, ni ajali za barabarani ikiwamo ya barabarani iliyopora maisha ya wanafunzi 13 na ile iliyosababisha vifo vya watu 14 wakiwamo wandishi wa habari watano mkoani Simiyu.

13 wakiwamo wanahabari watano wafa ajalini

Januari 11, mwaka huu, gari la waandishi wa habari lililokuwa kwenye msafara wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel liligongana uso kwa uso na Hiace na iliyokuwa na abiria eneo la Nyamikomo wilayani Busega katika Mkoa wa Simiyu.

Watu 14 walikufa wakiwemo waandishi wa habari watano huku zaidi ya 20 wakijeruhiwa.

Julai 26, gari la Shule ya Msingi ya King David iliyipo mkoani Mtwara lilitumbukia shimoni na kusababisha vifo vya watu 13 wakiwemo wanafunzi 11. Miongoni mwa wanafunzi hao ni watoto wawili wa familia moja. 

Ndege ya Precision Air inadondoka Ziwa Victoria

Novemba 6, 2022 wilayani Bukoba, Kagera, ndege ya Kampuni ya Precision Air ikaweka historia ya majonzi baada ya kudondoka ndani ya Ziwa Victoria.

Ajali hiyo ikasababisha vifo vya watu 19 huku wengine 28 wakinusurika baada ya kuokolewa.

Miongoni mwa watu waliofariki dunia ni pamoja na watumishi kutoka idara mbalimbali za Wizara ya Afya.

Kijana Majaliwa Jackson, mchuuzi wa samaki wilayani Bukoba, akaibuka shujaa katika ajali hiyo baada ya kuonesha ushujaa akiwa mstari wa mbele kwenda ilipoangukia ndege ndani ya ziwa na kushiriki kusaidia kufungua mlango wa ndege hiyo.

Hatua hiyo na ujasiri wake, vikasaidia kuokoa maisha ya abiria 28.

Ujasiri huo ukamfanya Rais Samia kuagiza kijana huyo apewe mafunzo na ajira katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com

Habari Zifananazo

Back to top button