MBUNGE wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, amesema mradi wa Shule ya Sekondari ambayo ni ya kwanza katika Kata ya Liwiti umeanza na Januari, 2023 wanafunzi wataanza masomo yao.
–
Bonnah ametoa taarifa hizo mara baada ya kutembelea miradi ya Kata ya Liwiti, akiambatana na Diwani wa Kata ya hiyo, Alice Mwangomo na Meya wa Jiji la Dar es Salaam ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Vingunguti, Omary Kumbilamoto.
–
Mbunge huyo ameeleza kuwa ujenzi wa soko la kisasa la Kata ya Liwiti umeanza na Januari soko hilo litaanza kufanya kazi. Amesema zaidi ya wafanyabiashara 200 watafanya shughuli zao katika eneo hilo.
–
“Ujenzi wa Daraja la Kwa Mzava, suala zima la bima za wazee kuisha muda wake linafanyiwa kazi. Mikopo ya asilima 10 ya Halmashauri, pamoja na suala zima la ulinzi shirikishi. Tunaanza zoezi la uboreshaji wa shule za msingi, ili ziweze kutoa elimu bora,” amesema Bonnah.
–
“Niombe wananchi tunapofanya mikutano hii wajitokeze kwa wingi kusikiliza nini serikali yao inafanya kwenye maeneo yao, pia watoe maoni na ushauri ili tuendelee kuboresha,”ameongeza Bonnah.