Mambo yameiva uvuvi wa kisasa

DAR ES SALAAM; NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, anatarajia kuzindua ‘App’ kwa ajili ya wavuvi wadogo ambayo itawasaidia kujua makundi ya samaki na wapi yalipo kupitia simu zao na kuachana na uvuvi wa kuwinda.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, wakati wa maadhimisho ya miaka 40 ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI).

Ulega amesema kuwa utafiti uliofanywa na TAFIRI na kuundwa kwa APP hiyo utasaidia wavuvi kuvua samaki kwa kutumia njia ya kisasa badala ya kubahatisha.

Amesema taasisi hiyo ni muhimili mzuri katika sekta ya uvuvi na hivi karibuni wamefanya mambo makubwa yaliyosababisha tija kwa wavuvi.

“Kesho (Alhamisi) Biteko moja ya mambo atakayoyafanya atazindua mfumo wa taarifa za wavuvi wadogo hili ni jambo kubwa ambalo tuliliagiza katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi na limekamilishwa,”amesisitiza Ulega.

Amesema, baada ya kukamilika kwa jambo hilo maana yake wanawaondoa wavuvi kwenye kuwinda samaki na wanapokwenda kuvua samaki watakuwa na taarifa kiganjani kupitia simu zao.

“Kupitia simu zao wataambiwa ni wapi yalipo makundi ya samaki umbali gani ili kumsaidia mvuvi kuweka mafuta yanayofanana na safari yake na kujua muda atakaoutumia, kwa sasa wavuvi wanakwenda kwa kubahatisha yaani wanawinda, unakuta anaweka mafuta ya Sh 20,000 anarudi na samaki wawili hii haikubaliki,”amesema.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button